PROF. NOMBO APONGEZA KASI YA UJENZI JENGO LA COSTECH DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 10, 2025

PROF. NOMBO APONGEZA KASI YA UJENZI JENGO LA COSTECH DODOMA



Na Edward Winchislaus,OKULY BLOG, DODOMA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Carolyne Nombo, ameeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa jengo jipya la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) linaloendelea kujengwa jijini Dodoma.

Akizungumza leo Septemba 10, 2025 mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Prof. Nombo amesema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 35, hali inayoonyesha umeenda mbele ya ratiba kwa asilimia 10 ikilinganishwa na lengo la awali la asilimia 25.

Ameeleza kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi Machi 2025 na unatarajiwa kukamilika Machi 2026, ambapo ukikamilika utakuwa chachu kubwa kwa vijana nchini katika kukuza na kuendeleza ubunifu wao.

"Kama mnavyojua, Taasisi hii ni mahususi katika kuratibu masuala ya sayansi na teknolojia. Kwa sasa inatumia ofisi zilizopo Dar es Salaam, lakini kwa maelekezo ya Serikali kwamba taasisi zote zihamie Dodoma, COSTECH imeanza rasmi ujenzi huu. Hapa vijana wataendelea kupata huduma za kukuza ubunifu wao sawa na ilivyokuwa Dar es Salaam," amesema Prof. Nombo.

Prof. Nombo amepongeza ubora wa ujenzi na kutoa wito kwa taasisi hiyo kusimamia kikamilifu ubunifu wa vijana ili bunifu zinazozalishwa ziwe na viwango vinavyokubalika na kuweza kushindana katika masoko ya ndani na ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema taasisi hiyo ina wataalamu wa kutosha wanaowaelekeza vijana namna bora ya kukuza ubunifu wao, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kuanzisha kampuni changa, kuwasajilia, kuwalipia kodi na kuwawezesha kujiajiri pamoja na kuwaajiri wengine.

Mradi huo unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 7.3 hadi kukamilika kwake na utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 600 kwa wakati mmoja.






No comments:

Post a Comment