
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Mabingwa watetezi wa mchezo wa netiboli na kuvuta kamba wanaume wote wanatoka Ofisi ya Rais Ikulu wametinga kibabe kwenye hatua ya nusu fainali baada ya kuwashinda wapinzani wao katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Michezo la Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI).
Ikulu netiboli ambao ni mabingwa wa kihistoria kwa kuwa mabingwa kwa kila mwaka waliwashinda TAMISEMI kwa magoli 81-26, hadi wanakwenda mapumziko washindi walikuwa mbele kwa magoli 45-12.
Timu zingine zilizoungana na Ikulu katika hatua ya nusu fainali ni Ofisi ya Ukaguzi walkiowafunga Wizara ya Ujenzi kwa magoli 48-40, hadi wakati wa mapumziko Ukaguzi waliongoza kwa magoli 24-15.
Nayo klabu ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora waliwashinda Mahakama kwa magoli 80-6; Utumishi waliongoza hadi mapumziko kwa magoli 45-6; wakati Wizara ya Maliasili na Utalii waliwashinda Wizara ya Elimu kwa kuwafunga magoli 35-31 na hadi mapumziko washindi walikuwa mbele kwa magoli 15-14.
Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume, mabingwa watetezi Ikulu waliwavuta Mahakama kwa mvuto 1-0; huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliwashinda Ofisi ya Waziri Mkuu Sera kwa mivuto 2-0; nao Wizara ya Uchukuzi waliwaliza Hazina kwa mvuto 1-0 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) waliwavuta Wizara ya Maji kwa 2-0.
Kwa upande wa wanawake timu ya Mahakama iliwavuta Wizara ya Uchukuzi kwa 1-0; huku RAS Tanga wakawashinda Mashtaka kwa mivuto 2-0; nao TAKUKURU waliwaadabisha TAMISEMI kwa 2-0 na RAS Geita waliwavuta Wizara ya Katiba na Sheria 2-0.
Nusu fainali itafanyika tarehe 13 Septemba, 2025 kwa michezo hiyo ya soka, netiboli na kuvuta kamba, ambapo pia kutafanyika mchezo wa karata.












No comments:
Post a Comment