Dkt. Biteko Ashiriki Umwagaji Zege Zahanati ya Butinzya, Apongeza Ushiriki wa Wananchi Katika Maendeleo - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, December 29, 2025

Dkt. Biteko Ashiriki Umwagaji Zege Zahanati ya Butinzya, Apongeza Ushiriki wa Wananchi Katika Maendeleo



Na Mwandishi Wetu, Bukombe


Mbunge wa Jimbo la Bukombe Dkt. Doto Biteko, leo ameshiriki na wananchi wa Kata ya Butinzya katika zoezi la umwagaji zege kwenye zahanati inayojengwa katika kata hiyo, akiwapongeza kwa moyo wao wa kujitolea na kushiriki moja kwa moja katika shughuli za maendeleo.

Dkt. Biteko aliambatana na viongozi wa Chama na Serikali ngazi ya wilaya pamoja na Diwani wa Kata hiyo, ambapo aliwaeleza wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inathamini ushirikiano na juhudi za wananchi katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Katika hotuba yake, Dkt. Biteko aliwapongeza wakazi wa Butinzya kwa kuonesha uzalendo kwa vitendo kwa kushiriki shughuli za ujenzi wa zahanati hiyo, badala ya kusubiri Serikali peke yake kuleta maendeleo.

“Maendeleo hayawezi kuletwa na Serikali pekee bila ushirikiano wa wananchi. Mmetuonesha mfano bora, na mimi nipo pamoja nanyi kila hatua kuhakikisha maendeleo Bukombe yanakuja kwa kasi na tija,” alisisitiza Dkt. Biteko.

Aidha, alitumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyoendelea kuijali wilaya ya Bukombe kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Mheshimiwa Rais ana nia ya dhati ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Kila tunapoomba fedha za miradi, amekuwa msikivu na kutenga fedha hizo kwa wakati,” alisema Dkt. Biteko.

Zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya karibu na wananchi na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za msingi, hasa maeneo ya vijijini.

No comments:

Post a Comment