DKT MWIGULU: TUACHE TABIA YA KUZOEA MATATIZO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, December 22, 2025

DKT MWIGULU: TUACHE TABIA YA KUZOEA MATATIZO


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewaonya watendaji na watumishi wa umma waache tabia ya kuzoea matatizo hasa katika sehemu zinazotoa huduma kwa wananchi.

Ametoa onyo hilo jana (Jumapili, Desemba 21, 2025) wakati akizungumza na wagonjwa na watumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi alipofanya ziara ya kushtukiza ili kujionea hali halisi ya utoaji huduma siku za wikiendi katika hospitali hiyo.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa na ratiba ya kukagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, mara baada ya kuwasili wilayani humo akitokea Ruangwa, aliamua kuanzia kwanza hospitalini kisha akaenda kwenye ukaguzi wa jengo hilo.

Akiwa hospitalini hapo, alienda moja kwa moja kwenye chumba cha daktari wa zamu ili apate utaratibu wa kumhudumia mgonjwa pindi anapofika hospitalini na akaelezwa kwamba ni lazima mgonjwa aanzie mapokezi na kukata cheti ndipo aje kwa daktari.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alikuta wagonjwa wawili nje ya vyumba vya madaktari ambao mmoja wao alikuwa na cheti lakini mwingine hakuwa nacho na alishapita mapokezi bila kuelezwa chochote. Na vyumba vya madaktari havikuwa na wagonjwa, licha ya kuwa madaktari walikuwemo.

“Wekeni utaratibu wa kuwaelekeza wagonjwa waende wapi mara tu wanapofika hospitalini. Hapa si mahali pa kuja kufanya matembezi, mtu akija hapa anahitaji kupewa huduma,” alisema wakati akiongea na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Ramadhani Mahiga.

“Naibu Waziri wa Afya toa maelekezo kwa hospitali zote, mgonjwa akifika hospitalini asikilizwe na kuelekezwa wapi pa kwenda. Akifika kwa daktari, kama hakuna mgonjwa mwingine, hana sababu ya kusubirishwa kama tulivyoona hapa,” alisema wakati akitoa maagizo kwa Dkt. Florence Samizi ambaye alikuwepo kwenye ziara hiyo.

“Kuna utaratibu wa kuzoea matatizo, kama kwenye chumba cha daktari hakuna mgonjwa au chumba kingine chochote hakuna mgonjwa, tusiweke mazoea ya kuwangojesha wagonjwa. Tuwahudumie mara moja. Tusidhani kwamba tunapowasubirisha sana, ndiyo sisi tumekuwa mabosi. Haya mambo ni ya huduma, tujirekebishe,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alikwenda eneo la maabara na kuzungumza na wagonjwa waliokuwa wakisubiri majibu yao ili kubaini kama kuna ucheleweshaji wowote wa utoaji huduma. Huko alielezwa utaratibu wa vipimo ukoje na muda wa kusubiri kwa baadhi ya vipimo.

Akiwa katika wodi ya wazazi, Waziri Mkuu aliwatembelea akinamama 12 waliokuwemo wodini, kuongea nao na kisha kupewa maelezo ya huduma zinazotolewa na hospitali hiyo. Akitoa maelezo hayo, mkunga na msimamizi wa wodi hiyo, Bw. Dennis Namwembe alisema kwa siku moja, akinamama kati ya sita hadi 10 wanajifungua hospitalini hapo na kwa mwezi mmoja wanaojifungua wanafikia 200.

“Kuhusu huduma ya upasuaji kwa akinamama wanaojifungua, idadi yao inaweza kufikia wastani wa 50 kwa mwezi,” Bw. Namwembe alimweleza Waziri Mkuu.

Vilevile, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga cha Nachingwea ambacho kipo jirani kabisa na hospitali hiyo ambako alielezwa kuwa ujenzi wake umesimama kwa sababu wanasubiri fedha za kukamilisha.


Dkt. Samizi alisema ujenzi wa chuo hicho unagharimiwa na Wizara ya Afya kwa gharama ya sh. bilioni 2.2 ambapo katika awamu ya kwanza, sh. milioni 900 zilikwishatolewa na kutumika.

“Katika awamu ya pili, wizara imetenga sh. bilioni 1.2 ambapo baada ya kukamilika, chuo hicho kinatarajia kuanza udahili wa wanafuzi kati ya 300 – 400 ifikapo Oktoba, 2026,” alisema.

Mapema asubuhi, Waziri Mkuu alikagua bandari ya Lindi iliyoko eneo la Barazani mjini Lindi na kuiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania ikamilishe masuala ya kitaalamu kuhusu bandari hiyo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Tellack alisema wanatamani bandari hiyo ifanyiwe ukarabati kwa kuongeza kina ili iweze kuhudumia meli nyingi zaidi kwani imeanza kuchangamkiwa na wafanyabiashara wakiwemo wa nchi jirani ambao huagiza vyakula na mifugo kutoka Tanzania.

“Mizigo inayopita hapa inafikia tani 1,000 kwa mwezi. Tuna ng’ombe wanatoka Kanda ya Ziwa, wanakaa hapa kwa muda mrefu hadi wanapoteza uzito, hii ni hasara kwa wauzaji.”

Kauli ya Mkuu wa Mkoa iliungwa mkono na Mbunge wa Lindi Mjini, Bw. Mohamed Utaly ambaye alisema anaomba bandari hiyo ikarabatiwe kwani ni nyenzo muhimu katika uchumi wa wana-Lindi. “Wakulima wanalazimika kupeleka korosho zao hadi Mtwara ambayo ni gharama kubwa kwao; kama bandari hii ingetumika, ingewapunguzia mzigo sana,” alisema.

No comments:

Post a Comment