DKT. SEIF AHIMIZA USIMAMIZI WA KARIBU MAJENGO YA KITUO CHA AFYA LWAMGASA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, December 21, 2025

DKT. SEIF AHIMIZA USIMAMIZI WA KARIBU MAJENGO YA KITUO CHA AFYA LWAMGASA


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif, ameuagiza Uongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Geita kusimamia kwa ukaribu ujenzi wa majengo matatu ya Maabara, Wodi ya Wazazi na Upasuaji, na jengo la wagonjwa wa nje OPD katika kituo cha afya Lwamgasa ili yakamilike kwa wakati na kuanza kutumika mapema kabla ya Machi 2026.

Dkt. Seif, ametoa agizo hilo Desemba 21, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi ya afya inayotekelezwa sehemu mbalimbali za Halmashauri ya Geita DC, mkoani Geita, ziara iliyoenda sambamba na kufanya mikutano ya hadhara akitoa fursa kwa wananchi kutoa maoni, mapendekezo na mitazamo yao juu ya mienendo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Dkt. Seif amesema kuwa, hitaji la kituo cha afya kwa Kata ya Lwamgasa ni kubwa na lenye kuhitaji uharaka, kutokana na zahanati ya Rwamgasa inayowahudumia wakazi wote wa Kata hiyo kuelemewa, ambapo idadi ya wajawazito wanaojifungulia katika zahanati hiyo ni wanawake 250 kwa mwezi, wakati Kata hiyo ina zaidi ya wakazi elfu 72.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Lwamgasa Mhe. Daniel Mabala amesema wakazi katika eneo hilo la Lwamgasa wanatazama kukamilika kwa kituo hicho kama uboreshaji mkubwa wa huduma za afya ya uzazi wa mama na mtoto jambo litakalosaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto wachanga.

Awali meneja mahusiano wa mgodi huo wa Buckreef Amelda Msuya ameipongeza Serikali ya Mkoa wa Geita kuelekeza zaidi ya shilingi milioni 320 kati ya milioni 600 zilizotolewa na mgodi huo kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa mwaka 2025/2026 ili kujenga nyumba za watumishi, wodi moja ya wagonjwa pamoja na miundombinu ya vyoo katika kituo hicho cha afya cha Lwamgasa.




No comments:

Post a Comment