
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Kanda ya Chamwino Leo Disemba 15, 2025 majira ya saa 3:00 asubuhi imemkamata Ndugu Gusha Lucas Mkazi wa Kitongoji cha Sokoine, Chamwino Ikulu kwa Wizi wa Maji kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2023.
Mteja huyo mwenye historia ya kujihusisha na wizi huo wa maji ya DUWASA kwa mara ya kwanza alifanya tukio hilo mwaka 2022 na kutakiwa kulipa faini ya shilingi 800,000 deni ambalo bado hajamaliza akidaiwa shilingi 400,000 zilizosalia.
Timu ya DUWASA-Chamwino imebaini wizi huo wa maji siku ya Ijumaa Disemba 12, 2025 wakati wakikifanya ukaguzi wa miundombinu yake na kugundua mteja huyo huyo ndio ameendelea na wizi wa maji kwa mara ya pili kwa kukata Bomba la Maji na kulificha kwa jiwe na kutumia maji kwa shughuli za kilimo za migomba, bustani ya mbogamboga na kutumia maji hayo ya wizi kwa kujengea.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Meneja wa DUWASA, Kanda ya Chamwino, Mhandisi Gray Mbalikila kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA amesema kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sokoine wamemfikisha mteja huyo kwenye vyombo vya dola kwa hatua za kisheria.
Mhandisi Gray amekemea tabia ya wizi wa maji unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wateja kuhujumu huduma za DUWASA na kusababisha upotevu wa maji.





No comments:
Post a Comment