
Na Meleka Kulwa – Dodoma
Mkurugenzi wa Miradi wa Habitat for Humanity Tanzania, John Massenza, amesema ujenzi wa vyumba vya vyoo vya kisasa katika minada ya Bahi na Kigwe utakapokamilika utaimarisha mazingira ya biashara, afya na usafi kwa wafanyabiashara pamoja na wananchi wanaotumia minada hiyo wilayani Bahi, mkoani Dodoma.
Massenza ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kukagua na kukabidhi maeneo ya ujenzi iliyofanyika Desemba 16, 2025, ambapo alikabidhi rasmi maeneo ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa wahandisi watakaosimamia ujenzi wa vyumba vya vyoo katika minada ya Bahi na Kigwe.
Amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa majengo ya vyoo vya kisasa pamoja na miundombinu rafiki kwa wanawake, ikiwemo jengo maalumu litakalowawezesha wanawake kujisitiri wanapokuwa na mahitaji maalumu.
Kwa mujibu wa Massenza, jumla ya vyumba 26 vya vyoo vitajengwa katika minada hiyo miwili, vikiwemo vyumba 10 kwa wanaume na 16 kwa wanawake. Kila mradi pia utakuwa na tanki la maji, chumba cha mahitaji ya wanawake, bafu, chumba cha wakina mama wanaonyonyesha pamoja na ofisi ya wasimamizi wa huduma.
Aidha, amebainisha kuwa katika kila mnada vitajengwa vyumba viwili maalumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu, hatua itakayoongeza ushirikishwaji na usawa katika matumizi ya huduma hizo.
Amesema mradi wa ujenzi wa vyoo katika Mnada wa Bahi utagharimu shilingi milioni 60, huku mradi wa Mnada wa Kigwe nao ukigharimu shilingi milioni 60, na kwamba miradi hiyo inatarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 4,000 itakapokamilika.
Katika mpango wa uendeshaji, Massenza amesema watumiaji wa vyoo watalipia huduma kwa kiwango kidogo ili kugharamia matengenezo, uendeshaji wa miradi pamoja na kuchangia kuboresha makazi ya wananchi na kuongeza kipato chao.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuboresha afya na ustawi wa jamii, kuongeza kipato cha wananchi na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia mazingira bora ya biashara na upatikanaji wa huduma muhimu za usafi wa mazingira.
Habitat for Humanity inafanya kazi katika zaidi ya nchi 70 duniani, ikiwa na makao makuu nchini Marekani. Massenza amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo katika kuboresha huduma za vyoo na usafi wa mazingira katika maeneo ya minada na jamii kwa ujumla.
Katika ziara hiyo, Massenza aliambatana na viongozi wa serikali za vijiji na mitaa pamoja na maafisa mazingira kutoka Wilaya ya Bahi.
Awali, mhandisi wa mradi alisema kuwa kila tanki la maji litakuwa na ujazo wa lita 3,000, huku ujenzi wa majengo hayo ukitarajiwa kuchukua kati ya wiki nane hadi kumi, na kwamba mradi mzima unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 90.







No comments:
Post a Comment