
Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
Wakala ya Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) leo, Desemba 16, 2025, imetekeleza zoezi la ufunguzi wa zabuni za uagizaji mafuta kwa ajili ya mahitaji ya mwezi Februari, 2026 ambapo kampuni 8 kati ya 11 zimeshinda zabuni hizo katika vipengele tofauti.
Zoezi hilo limefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa PBPA jijini Dar es Salaam, likihusisha wazabuni wa kimataifa na wa ndani, pamoja na wadau wa sekta ya nishati.
Ufunguzi huo ni sehemu ya utaratibu wa kisheria na kikanuni wa kuhakikisha nchi inakuwa na nishati ya Mafuta ya kutosha na ya uhakika, huku ikizingatia misingi ya uwazi, ushindani wa haki, na gharama nafuu kwa mlaji wa mwisho.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa PBPA, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Petroli, Wakala ya Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mhandisi Bruno Tarimo amewapongeza washindi wa zabuni hizo.
"Nawapongeza wazabuni wote mlioshinda. Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, ninasisitiza kwa wasambazaji wote walioshinda zabuni zao kukamilisha taratibu na masharti ya mikataba ili kufanikisha uingizaji wa mafuta kwa mfumo wa uagizaji wa pamoja (BPS) kwa mwezi Februari 2026 unafanyika kwa ufanisi." amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya zabuni ya Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS), Bw. Ali Saeed aliongoza zoezi la ufunguaji wa Zabuni na kuwatangaza washindi kisha kuwapongeza kwa ushindi huo.
Zoezi hilo limehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Wazabuni waliokidhi vigezo vya awali, Wawakilishi wa kampuni za uuzaji wa mafuta (OMCs) na Wadau wengine muhimu.





No comments:
Post a Comment