
Na Angela Msimbira , Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, leo Desemba 29, 2025, ameongoza kikao kazi maalum cha uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Idara, Vitengo na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.
Kikao hicho kinachofanyika jijini Dar es Salaam kimewakutanisha viongozi waandamizi wa TAMISEMI, Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na wawakilishi wa Taasisi husika, ambapo kila taasisi imewasilisha taarifa ya kina kuhusu hali ya utekelezaji wa miradi inayosimamia.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Prof. Shemdoe amesema lengo la kikao hicho ni kupokea, kuchambua na kujadili taarifa za miradi, kubaini hatua zilizofikiwa, kiwango cha matumizi ya fedha, changamoto zinazojitokeza pamoja na mikakati ya kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia ubora.
Ameeleza kuwa uwasilishaji wa taarifa sahihi na za wakati ni msingi wa maamuzi bora ya Serikali, akisisitiza kuwa taarifa hizo zinapaswa kuonesha kwa uwazi hali halisi ya utekelezaji wa miradi ili kusaidia Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kuchukua hatua stahiki mapema.
“Mnatakiwa kuwasilisha taarifa zinazoakisi uhalisia wa miradi iliyopo kwenye maeneo yenu, ikiwa ni pamoja na mafanikio, changamoto na hatua zinazochukuliwa kuzitatua. Taarifa hizi ndizo zitakazotusaidia kuboresha usimamizi wa miradi na kuwajibisha wahusika,” amesema Prof. Shemdoe.



No comments:
Post a Comment