SERIKALI YAWAASA VIJANA KUTUMIA FURSA ZINAZOPATIKANA KUTOKANA NA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, December 19, 2025

SERIKALI YAWAASA VIJANA KUTUMIA FURSA ZINAZOPATIKANA KUTOKANA NA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO


Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), (mwenye joho jekundu), akiongoza Maandamano ya Kitaaluma, wakati wa Mahafali ya 11 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika yaliyofanyika Katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere ambapo Mhe. Luswetula, alikuwa Mgeni Rasmi.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akizungumza na wahitimu na washiriki wa Mahafali ya 11 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika yaliyofanyika Katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha J ulius Nyerere.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akimtunuku mmoja wa wahitimu katika mahafali ya 11 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha J ulius Nyerere

Baadhi ya wahitimu wakila kiapo cha utii mara baada ya kutunukiwa ngazi mbalimbali za cheti katika mahafali ya 11 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Baadhi ya wahitimu wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), katika mahafali ya 11 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Meza kuu ikiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), ikiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa ngazi ya shahada ya uzamili katika Takwimu rasmi, katika mahafali ya 11 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha J ulius Nyerere.

Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Dkt. Indiale Daniel Kaaya, akizungumza na wahitimu na washiriki wa Mahafali ya 11 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika yaliyofanyika Katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), (mwenye joho jekundu) akisalimiana na Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Dkt. Indiale Daniel Kaaya mara baada ya kuwasili katika Mahafali ya 11 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika yaliyofanyika Katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Fadha-Dar es Salaam)


Na. Ramadhani Kissimba, WF – Dar es Salaam


Serikali imewataka vijana wanaohitimu masomo katika vyuo mbalimbali nchini kutumia fursa zinazopatikana kutokana na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuweza kuendeleza maisha watakapokuwa wakifanya shughuli mbali mbali za kiuchumi kwenye sekta binafsi na sekta ya umma.

Hayo yalibainishwa jijini Dar es salaam, na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) katika Mahafali ya 11 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika yaliyofanyika katika Kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Mhe. Luswetula alisema kuwa mabadiliko makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano yaani TEHAMA yanayojiri sehemu mbalimbali duniani na hata barani Afrika ambayo kwa sasa yamepewa jina la mapinduzi ya viwanda ya kizazi cha nne (Fouth Industrial Revolution) yamebadili kwa kiasi kikubwa uzalishaji mali katika uchumi na utoaji wa huduma za Umma kupitia mifumo ya kidijitali.

‘’Mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano yanabadili kwa kiasi kikubwa uzalishaji mali katika uchumi na utoaji wa huduma za umma kupitia mifumo ya kidijitali. Nitaje mifano michache kama vile biashara mtandaoni, elimu mtandaoni na kilimo cha kisasa kinachoendeshwa na mifumo ya kidijitali katika kufuatilia ukuzaji, ubora na uuzaji wa mazao ya kilimo na mifugo katika masoko ndani na nje ya nchi’’.Alisema Mhe. Luswetula

Aidha, Mhe. Luswetula aliwataka wahitimu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika na vijana kwa ujumla kuongeza nguvu katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na mazingira ya mabadiliko ya kidijitali na kuzigeuza changamoto hizo kuwa fursa za kuongeza ufanisi wa utoaji huduma, kukuza masoko pamoja na kuhimili ushindani kwenye soko.

Mhe. Luswetula pia alitoa rai kwa wadau wa sekta binafsi hususani rika la vijana, walio masomoni, wahitimu na walioko makazini, kuwekeza zaidi katika sekta ya ubunifu wa mifumo ya biashara kidijitali katika sekta wanazofanyia kazi.

‘’Tukumbuke pia mwelekeo wa sera ya elimu ni kukuza ubunifu, na hatimaye uzalishaji katika sekta mbali mbali pamoja na uwezo wa vijana kujiajiri na kutengeneza ajira. Yapo pia maboresho ya sera na sheria mbali mbali kama vile sheria za haki miliki, sera za uwezeshaji mitaji kwa makundi mbali mbali ya jamii yote yakilenga kuleta nafuu katika sekta hizo’’ aliongeza Mhe. Luswetula.

Awali akizungumza katika Mahafali hayo kwa niaba ya Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Dkt. Tumaini Katunzi, Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Dkt. Indiale Kaaya alisema Katika mwaka wa masomo 2024/2025, Chuo kimetekeleza majukumu yake ya ufundishaji, utafiti na kutoa huduma za kiushauri ambapo Chuo kimekamilisha na kufanya udahili na ufundishaji wa programu mpya ngazi ya shahada ya kwanza ya Acturial Science. Chuo pia kimeandaa utaratibu wa ufundishaji kozi zake kupitia elimu masafa kwa njia ya mtandao.

Dkt. Kaaya aliongeza kuwa sambamba na elimu Masafa, Chuo kimeendelea kuwekeza katika ujuzi na utaalamu katika masuala ya sayansi ya Data na TEHAMA ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya kasi ya uelimishaji vyuoni na ongezeko la mifumo ya kidijitali na akili mnemba kutumika kwenye mafunzo.

Dkt. Kaaya aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kufanikisha Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kutoka huduma za elimu kwa muda wa miaka sitini toka kuanzishwa kwake ambapo kwa sasa chuo kinahudumia nchi takribani 19 barani Afrika.

‘’Nipende kuchukua nafasi hii kudokeza kuwa tarehe 30 mwezi Agosti mwaka huu, 2025, Chuo kilitimiza miaka sitini tangu kuanzishwa kwake hapa Dar es salaam Tanzania na hadi mwaka huu chuo kinahudumia nchi wanachama kumi na tisa (19). Nichukue nafasi hii kushukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha ambayo imeendelea kukilea na kugharamikia Chuo hiki kwa niaba ya nchi wanachama.’’ Alisema, Dkt. Kaaya

Katika mahafali ya 11 ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika jumla ya wahitimu 312 walitunikiwa shahada ya Umahili, Stashahada ya Uzamili, Shahada ya awali, Diploma ya Juu na stashahada katika Takwimu rasmi, Takwimu za Kilimo, Takwimu za Biashara na Uchumi, Takwimu za Kilimo na Uchumi na Shahada ya Sayansi ya Data.

No comments:

Post a Comment