TANROADS: Kipande cha Barabara Kinachosambaa Mitandaoni Ni cha Majaribio - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, December 15, 2025

TANROADS: Kipande cha Barabara Kinachosambaa Mitandaoni Ni cha Majaribio



Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA


Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma umeeleza kuwa kipande cha barabara kinachosambaa katika mitandao ya kijamii kikionekana kujengwa chini ya viwango ni sehemu ya majaribio iliyojengwa kwa mujibu wa taratibu za kitaalamu kabla ya kuanza ujenzi kamili wa barabara husika.

Akizungumza jijini Dodoma, Mkuu wa Idara ya Matengenezo TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Elisony Edward Mweladzi, amesema kipande hicho chenye urefu wa takribani mita 300 kilijengwa mahsusi kwa ajili ya kufanya majaribio kabla ya kuwekwa tabaka la mwisho la lami, hatua ambayo ni ya kawaida katika miradi ya ujenzi wa barabara.

Ameeleza kuwa baada ya kufanyiwa vipimo na maabara ya TANROADS, ilibainika kuwa kipande hicho hakikukidhi viwango vilivyokubaliwa, hali iliyosababisha TANROADS kumwandikia barua mkandarasi anayetekeleza mradi huo akimtaka kuanza mara moja kufanya marekebisho ya kasoro zilizobainika, ikiwemo kukiondoa kabisa kipande hicho.

“Marekebisho ya kipande hicho yataanza Desemba 15, 2025, kabla ya kuendelea na hatua nyingine za ujenzi,” amesema Mhandisi Elisony.

Kwa upande wake, mkandarasi wa mradi huo, Mhandisi Edward Njau kutoka kampuni ya Kings Builders Company Limited, amethibitisha kupokea maelekezo kutoka TANROADS na kusema taratibu za marekebisho tayari zimeanza.

Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 7 utakapokamilika, huku TANROADS ikisisitiza kuwa itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wake ili kuhakikisha unazingatia viwango vya ubora na kutoa thamani halisi ya fedha za umma.

No comments:

Post a Comment