WANANCHI NZALI WAISHUKURU SERIKALI KWA UJENZI WA DARAJA LA SH. BILIONI 14.5 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, December 22, 2025

WANANCHI NZALI WAISHUKURU SERIKALI KWA UJENZI WA DARAJA LA SH. BILIONI 14.5




Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG , Chamwino – Dodoma


WANANCHI wa Kijiji cha Nzali, Kata ya Chilonwa wilayani Chamwino mkoani Dodoma, wameishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja ambalo limeondoa adha ya kukosa mawasiliano kwa muda mrefu, hususan nyakati za mvua ambapo baadhi ya wananchi walikuwa wakisombwa na maji na kukosa huduma muhimu za kijamii kama afya.

Shukrani hizo zimetolewa leo Desemba 22, 2025 katika hafla ya makabidhiano ya daraja hilo lenye urefu wa mita 60, lililofikia hatua ya ukamilishaji kwa asilimia 98 na linatarajiwa kukamilika rasmi Desemba 30 mwaka huu.

Wakizungumza kwa niaba ya wananchi, wamesema uwepo wa daraja hilo utarahisisha usafiri na usafirishaji, kuongeza fursa za biashara na kuimarisha shughuli mbalimbali za kiuchumi, jambo litakalosaidia kuinua kipato cha kaya na kuchochea maendeleo ya kijiji.


Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nzali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametoa ruhusa ya kuanza kutumika kwa daraja hilo licha ya kuwa katika hatua za mwisho za ukamilishaji.

Ameeleza kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi ili kuboresha miundombinu ya usafiri na kuondoa vikwazo vya maendeleo kwa wananchi.

“Mnatakiwa kulitumia daraja hili kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na biashara ili kujiondoa katika umaskini. Serikali imefanya yake, sasa ni zamu yenu kunufaika na fursa zinazotokana na uwepo wa miundombinu hii,” amesema Senyamule.

Awali, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo mkubwa ambao umegharimu jumla ya Shilingi bilioni 14.5.

Amesema mradi unasimamiwa na TANROADS chini ya Mkandarasi CHICO, na umejengwa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya usalama na uimara wa muda mrefu.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutaimarisha mawasiliano kati ya Kijiji cha Nzali na maeneo mengine ya wilaya ya Chamwino, kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na masoko ya mazao ya wakulima.

Daraja la Nzali ni sehemu ya jitihada za Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja nchini, hususan maeneo ya vijijini, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.



No comments:

Post a Comment