WAZIRI MCHENGERWA AZIKARIBISHA JUMUIYA ZA KIMATAIFA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KUBORESHA TIBA ASILI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, December 19, 2025

WAZIRI MCHENGERWA AZIKARIBISHA JUMUIYA ZA KIMATAIFA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KUBORESHA TIBA ASILI



Na John Mapepele, New Delhi.


Waziri wa Afya Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa amezikaribisha jumuiya za kimataifa na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya duniani kushirikiana na Tanzania katika kufanya tafiti, ubunifu na uhamishaji wa teknolojia, pamoja na biashara ya kimaadili ya tiba asili ili kuboresha huduma ya tiba asili kwa kuwa tiba asilia inaweza kuwa nguzo muhimu ya afya bora na maendeleo endelevu ya kiuchumi duniani.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo wakati akiwasilisha uzoefu wa Tanzania kwenye mada ya tatu iliyohusu “kufikiria upya mifumo ya afya kwa usawa, usalama na ustahimilivu katika eneo la Tiba Asili” kwenye Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu Tiba Asilia, unaoendelea jijini New Delhi nchini India.

“Tanzania inaendelea kubadilisha tiba asilia kutoka katika mfumo wa jadi Kwenda katika mfumo wa tiba yenye ushahidi wa kisayansi, inayodhibitiwa kitaalamu, inalindwa kidijitali, na yenye mchango wa kiuchumi. Kwa sasa takribani asilimia 60 ya watanzania hutegemea tiba asilia, huku zaidi ya waganga 60,000 na vituo zaidi ya 2,000 vikisajiliwa rasmi nchini”. Amefafanua Waziri Mchengerwa.

Ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania inaweka mkazo katika utafiti wa gharama nafuu unaozingatia jamii, pamoja na uthibitishaji wa usalama, ubora na ufanisi wa tiba asili, sambamba na utekelezaji wa Mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa Tiba Asili wa mwaka 2025–2034 ambapo amesisitiza kuwa Tanzania hailegezi udhibiti wa tiba asilia, bali inaiboresha kitaaluma kupitia mifumo imara ya sheria na taasisi za udhibiti.

Akizungumzia ujumuishaji wa tiba asilia katika mifumo ya afya, Waziri Mchengerwa ameeleza kwamba, Tanzania imeanza kutumia huduma za tiba asili katika vituo vya afya, ambapo hadi sasa bidhaa 27 za tiba asilia zimetumika katika utoaji wa huduma za afya tangu mwaka 2023 huku akisisitiza kuwa ujumuishaji wa tiba asili katika mifumo ya afya si ushindani, bali ni ushirikiano, unaolenga kufanikisha Bima ya Afya kwa Wote.

Katika eneo la maendeleo ya kiuchumi, Mheshimiwa Mchengerwa amebainisha kuwa Tanzania imesajili bidhaa 141 za tiba asilia, ambapo zaidi ya asilimia 90 huzalishwa na wazalishaji wadogo wa ndani, hatua inayochangia ajira na kukuza uchumi na kwamba Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuhimiza ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, kilimo cha mimea tiba, usindikaji, na upatikanaji wa masoko ya ndani na ya kimataifa.

Pia amesisitiza umuhimu wa kulinda haki miliki na maarifa ya jadi ya jamii, pamoja na matumizi ya akili mnemba (AI) na teknolojia za kidijitali kuhifadhi, kuthibitisha, na kulinda maarifa ya tiba asili. Vilevile, alieleza kuwa teknolojia haitachukua nafasi ya waganga wa jadi, bali itaongeza na kulinda hekima yao.

Mkutano huo wa siku tatu unatarajiwa kufungwa na leo na Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi, jambo linaloonesha uzito na umuhimu mkubwa wa mkutano huo katika ngazi ya juu ya kisera.






No comments:

Post a Comment