WAZIRI NYANSAHO AFUNGUA BARAZA LA WAFANYAKAZI WIZARA ULINZI NA JKT MOROGORO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, December 18, 2025

WAZIRI NYANSAHO AFUNGUA BARAZA LA WAFANYAKAZI WIZARA ULINZI NA JKT MOROGORO



Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho,(Mb) tarehe 18 Desemba 2025 amefungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, katika Ukumbi wa Umwema mkoani Morogoro.

Kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na JKT, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, kilihudhuriwa na wajumbe kutoka Wizara, Ngome na JKT pamoja na ujumbe wa Tughe Taifa wa Morogoro.

Akizungumza kwenye ufunguzi huo, Waziri wa Ulinzi, Dkt Nyansaho, amewaeleza washiriki wa Baraza la Wafanyakazi kuwa
Kukusanyika kwao ni sehemu muhimu katika kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi na tija katika Taasisi yetu. Akawaambia kuwa uzoefu umeonesha kuwa, Mabaraza ya Wafanyakazi yanapotumika vyema, huleta hali ya maelewano, umoja, ushirikiano na utulivu mahali pa kazi.

Aidha, akawaasa kutambua kuwa, ushirikiano wenye tija unahitaji nidhamu, uwajibikaji na moyo wa kujituma. "Tunapofanya kazi kwa umoja, tunapaswa kuhakikisha kuwa, kila mmoja wetu anatimiza wajibu wake ipasavyo, kwa uaminifu na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma" alisisitiza Dkt Nyansaho.

Waziri wa Ulinzi na JKT amewaeleza washiriki hao wa Baraza kuwa, katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kama Watumishi wa Umma, hatuwezi kuepuka changamoto mbalimbali zinazoathiri utendaji kazi wetu, hivyo ni vyema changamoto zinazojitokeza zitatuliwe kwa hekima na busara.

Akaongeza kwa kueleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, imeendelea kushughulikia changamoto mbalimbali za watumishi wa umma ikiwemo kulipa malimbikizo mbalimbali ya watumishi na kuwapandisha vyeo kwa wakati watumishi wenye sifa ili kuhakikisha malengo ya serikali na taasisi za umma yanafikiwa kwa ufanisi.

Waziri wa Ulinzi Mhe Dkt Rhimo Nyansaho akahitimisha kwa kutoa wito kwa watumishi wote wa Wizara anayoiongoza kuzingatia masuala muhimu kwa umakini kwa
kufanya kazi kwa Uadilifu, kuepukana na rushwa na pia
kila mtumishi ajilinde na Maambukizi ya Ugonjwa wa VVU/UKIMWI kwa kuepuka tabia hatarishi. Vilevile, akawataka kufanya mazoezi ya mwili kwa ajili ya kuimarisha afya na kuepuka Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (MSY).





No comments:

Post a Comment