![]() |
| Kaimu mkurugenzi wa BOT kanda ya Mwanza Amon Mwambonda akizungumza wakati wa mafunzo ya fedha kwa wachimbaji wadogo na wa kati wilayani Kahama yaliyoandaliwa na benki kuu ya Tanzania (BOT). |
![]() |
| Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wachimbaji wadogo na wa kati wilayani humo yaliyoandaliwa na benki kuu ya Tanzania (BOT). |
Benki Kuu ya Tanzania (BOT), imewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini kutumia mifumo rasmi ya malipo ili kuongeza usalama wa fedha zao, kuboresha biashara na kujijengea historia ya miamala itakayorahisisha upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za kifedha.
Akizungumza katika mafunzo ya elimu ya fedha kwa wachimbaji wadogo na wa kati wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Latifah Mikoyi kutoka BOT, anayesimamia mifumo ya malipo amesema, matumizi ya mifumo rasmi ya malipo hupunguza utegemezi wa fedha taslimu.
Amesema mifumo hiyo pia inaondoa hatari ya wizi, upotevu na changamoto nyingine za usalama.
Amesema kupitia teknolojia ya kifedha, wachimbaji wanaweza kufanya miamala kwa kutumia simu za mkononi, huduma za kibenki kwa njia ya simu (mobile banking) pamoja na njia nyingine za kidijitali bila ulazima wa kubeba fedha taslimu.
“Mfumo wa malipo unamsaidia mchimbaji kupokea malipo kwa haraka kutoka kwa wanunuzi wa madini, kulipa wafanyakazi kwa urahisi na kuepusha matumizi ya cash ambayo yanaweza kuwa na hatari,” alisema Mikoyi.
Mikoyi amesema matumizi ya mifumo rasmi ya malipo huwasaidia wachimbaji kujenga rekodi za kifedha, jambo ambalo ni muhimu wanapotaka kuomba mikopo kwenye benki na taasisi nyingine za fedha.
“Wachimbaji wengi wanakosa mikopo kwa sababu hawana taarifa rasmi za biashara zao, kwani hutumia cash pekee. Wakianza kutumia mifumo rasmi ya malipo, miamala yao itaonekana na itawasaidia kukopesheka,” aliongeza.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Mukrim Ramadhan kutoka BOT, amesema Taifa lenye wananchi wenye uelewa mkubwa wa masuala ya fedha, lina nafasi kubwa ya kufikia maendeleo ya haraka na endelevu.
Amesema “Wachimbaji wadogo wanahitaji vifaa vya gharama kubwa ili kufanya kazi kwa ufanisi, lakini mara nyingi sera za mikopo zilizopo katika benki za biashara hazikidhi mahitaji yao.”
Wachimbaji wadogo wa madini na wadau wa sekta hiyo Wilayani Kahama wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kubadili mtazamo wa matumizi ya fedha, kuweka akiba na kuwekeza kwa manufaa ya baadaye.
Akifungua mafunzo hayo, mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, (BOT) kwa kuandaa mafunzo hayo na kwamba ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa wananchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Amesema ili wananchi wafikie maendeleo ya kweli ni lazima wawe na uelewa wa masuala ya fedha na namna bora ya kutumia rasilimali walizonazo.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuinua uchumi wa wananchi, kuboresha ustawi wa familia na kujenga taifa lenye nguvu kiuchumi.
“Kwa kufikia maendeleo tunayoyataka lazima tuwe na elimu ya fedha katika jamii. Hili ni wazo zuri sana na tunawapongeza BOT kwa kuchagua Wilaya ya Kahama kwa mafunzo haya muhimu,” amesema Nkinda.
Aidha amesisitiza kuwa elimu hiyo itasaidia kubadilisha maisha ya wachimbaji na familia zao, huku akieleza matumaini kuwa maarifa yatakayopatikana yatachochea mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika jamii ya Kahama na maeneo jirani.







No comments:
Post a Comment