Na Mwandishi Wetu, Tabora
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 30 Aprili, 2026 katika ofisi za mkuu wa mkoa wa Tabora, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema, Mamlaka iko kwenye operesheni maalum ya kuteketeza dawa za kulevya zinazozalishwa nchini.
“Sasa hivi tuko kwenye kampeni maalum kuhakikisha kwamba tunateketeza dawa za kulevya zinazozalishwa nchini baada ya dawa za viwandani kupungua” amesema Lyimo.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Mamlaka kuanzisha ofisi za DCEA kanda ya Magharibi yenye makao yake mkoani Tabora, hatua ambayo imeongeza ufanisi na kasi katika kudhibiti dawa za kulevya nchini.
Sambamba na hilo, Kamishna Jenerali Lyimo ameushukuru uongozi wa mkoa kwa kuunga mkono na kushiriki operesheni hiyo iliyofanikisha ukamataji na uteketezaji wa bangi zinazolimwa katikati ya mapori na hifadhi za taifa mkoani humo.
“Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya hatutakubali uhalifu huu uendelee. Tutahakikisha tunafanya operesheni endelevu katika maeneo yote na kuchukua hatua za makusudi kwa watu wanaolima na kuzalisha dawa za kulevya ndani na nje ya mapori” amesisitiza Lyimo.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Tabora Dkt. Paul Chacha, ameipongeza Mamlaka kwa kazi nzuri ya udhibiti wa dawa za kulevya inayoendelea mkoani humo na kuwaagiza askari wa TFS kuweka kambi katika mapori na maeneo ya hifadhi ili kumaliza kabisa tatizo la bangi katika mkoa wa Tabora.








No comments:
Post a Comment