DOLA ZA MAREKANI BILIONI 1.28 KUJENGA SGR KIPANDE CHA MAKUTUPORA–ISAKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, April 28, 2026

DOLA ZA MAREKANI BILIONI 1.28 KUJENGA SGR KIPANDE CHA MAKUTUPORA–ISAKA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali imesaini mkataba wa dola za Marekani bilioni 1.277 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) kipande cha Makutupora–Isaka, hatua inayotarajiwa kuharakisha ujenzi wa mtandao wa reli ya kisasa nchini.

Mkataba huo umesainiwa Aprili 28, 2026 jijini Dodoma, ukihusisha ujenzi wa kipande cha Lot 3 na 4 chenye jumla ya kilometa 533, ikijumuisha Makutupora hadi Tabora (km 368) na Tabora hadi Isaka (km 165).

Hafla ya utiaji saini ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, taasisi za kifedha, mabalozi na wadau wa maendeleo, ambapo Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Dkt. Khamis Mussa Omar alikuwa mgeni rasmi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Omar amesema jumla ya taasisi tatu za kifedha kutoka Italia, Sweden na Poland zimefadhili mradi huo kwa dola bilioni 1.277, huku akibainisha kuwa utekelezaji wake tayari umeanza.

Amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa ujenzi wa reli ya SGR, ambapo kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma tayari kimekamilika na kinafanya kazi, huku kipande cha Isaka hadi Mwanza kikiwa kinaendelea kujengwa na Tabora hadi Kigoma nacho kimeanza.

“Ufadhili huu utasaidia kukamilisha ujenzi wa reli ya kisasa yenye jumla ya kilometa zaidi ya 2,100, ambayo ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi,” amesema Dkt. Omar.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni hatua muhimu ya kihistoria itakayoifanya Tanzania kuwa kitovu cha kisasa cha usafirishaji na usambazaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Amesema tangu kuanza kwa mradi wa SGR mwaka 2017, zaidi ya kilometa 2,100 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi, huku kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma kikiwa tayari kimeshasafirisha zaidi ya abiria milioni tano.

“Mradi huu umechangia kupunguza muda wa safari, gharama za usafiri na kiwango cha hewa ya ukaa kwa zaidi ya asilimia 50, sambamba na kuongeza ajira kwa Watanzania,” amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, ameongeza kuwa kukamilika kwa kipande cha Makutupora–Isaka kutafungua fursa mpya za biashara, ajira na kuimarisha maendeleo ya kikanda.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba aliwashukuru wadau wa maendeleo kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, huku washirika hao wakiahidi kuendeleza ushirikiano huo.

Kwa upande wao Mabalozi wa nchi za Sweden, Mhe. Charlotta Marcias, Balozi wa Italia, Mhe. Giuseppe Sean Coppola na Mwakilishi wa Balozi wa Poland nchini, Bw. Sergiusz Wolski, wamesema kuwa wameridhishwa na uendelezaji wa mradi wa reli ya kisasa (SGR), na kueleza kuwa ni kielelezo cha uhusiano imara wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi hizo ambapo mafanikio yaliyopatikana katika Loti ya 1 na 2 yamefungua milango ya ushirikiano mpana zaidi katika loti zinazofuata.

Walisisitiza kuwa kupitia taasisi zao za kifedha na mashirika ya mikopo, wataendelea kusaidia miradi mikubwa ya miundombinu inayozingatia uendelevu na viwango vya kimataifa huku wakibainisha kuwa ushirikiano huo utafungua milango kwa kampuni zaidi za Ulaya kuwekeza nchini na kuchangia ukuaji wa sekta binafsi pamoja na ajira.






No comments:

Post a Comment