FEMATA YAJIPANGA KUWAINUA WACHIMBAJI KWA UJUZI WA KISASA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 29, 2026

FEMATA YAJIPANGA KUWAINUA WACHIMBAJI KWA UJUZI WA KISASA


Rais wa FEMATA, John Bina amesema safari ya mafunzo na kubadilishana ujuzi iliyofanywa na shirikisho hilo huko Ontario, Canada ni sehemu ya juhudi za kuifanya sekta ya wachimbaji wadogo na wa kati nchini kuwa ya kisasa na yenye tija zaidi.

Akizungumza katika mahojiano maalum yaliyofanyika, jijini Dodoma, Bina amesema safari hiyo haikuwa ya matembezi bali ilikuwa na lengo la kujifunza kwa vitendo na kurejesha maarifa yatakayosaidia kuboresha shughuli za uchimbaji nchini.

“Safari hii si ya matembezi; ni ya kuhamisha maarifa ya vitendo kwa wachimbaji wa Tanzania,” alisema Bina.

Amesema sekta ya madini inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi, ikichangia takribani asilimia 10.1 ya Pato la Taifa, huku mauzo ya dhahabu nje yakizidi dola za Marekani bilioni nne kwa mwaka. Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wachimbaji wadogo hawaachwi nyuma katika matumizi ya teknolojia, usalama kazini, uchakataji wa madini na upatikanaji wa masoko.

Bina ameeleza kuwa ujumbe wa FEMATA ulipata fursa ya kujionea mifumo ya kisasa ya uchakataji madini, ikiwemo mikanda ya kusafirisha malighafi, mashine za kuchuja na kupanga madini, pamoja na mifumo ya usalama na vifaa vya kisasa vya viwandani.

Amebainisha kuwa uzoefu huo utasaidia kuongeza uzalishaji, kupunguza upotevu wa madini na kuboresha ubora wa madini kabla ya kuuzwa katika masoko ya kimataifa.

Aidha, amesema hatua inayofuata ni kuandaa programu za mafunzo kwa wachimbaji katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji ikiwemo Geita, Chunya, Kahama, Shinyanga na Mara.

Ameongeza kuwa kuboreshwa kwa mafunzo, usalama kazini na uanzishwaji wa vituo vya pamoja vya uchakataji kutaiwezesha Tanzania kuongeza thamani ya madini kabla ya kuyauza nje, na hivyo kuifanya sekta hiyo kuwa rasmi zaidi, yenye tija na manufaa kwa wachimbaji pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment