Na Gladys Lukindo, Manyara
Madaktari bingwa wa upasuaji wamefanikiwa kumuondoa mwanamke uvimbe wenye uzito wa kilo mbili uliokuwa mgongoni mwake kwa zaidi ya miaka 10, hali iliyokuwa ikimsababishia maumivu makali.
Akizungumza baada ya upasuaji huo, Daktari Bingwa wa Upasuaji, Sandra Sillas, amesema mgonjwa huyo alikuwa akipata maumivu yanayokuja na kupotea kwa muda mrefu kutokana na uvimbe huo mkubwa.
“Uvimbe tuliouondoa ulikuwa mgongoni na ulikuwa na uzito wa kilo mbili. Hali hii ilikuwa hatari kiafya kwa mgonjwa,” amesema Dkt. Sandra.
Ameongeza kuwa kama uvimbe huo usingeondolewa mapema, ungeendelea kukua na hatimaye kusababisha madhara makubwa zaidi, ikiwemo uwezekano wa kugeuka saratani.
“Uvimbe huu ulikuwa umeendelea kukua kwa zaidi ya miaka kumi, na kama usingetolewa ungeweza kusababisha madhara makubwa zaidi kwa mgonjwa,” amefafanua.
Kwa upande wake, mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huo aliishukuru timu ya madaktari kwa huduma aliyopatiwa, akisema kabla ya matibabu alikuwa anakumbwa na changamoto kubwa ya kulala na hata kuegemea.
“Kabla ya upasuaji sikuweza kulala wala kuegemea vizuri, lakini sasa hali yangu inaendelea kuimarika. Nawashukuru sana madaktari kwa kunisaidia,” amesema.
Upasuaji huo umefanywa na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, ambao kwa sasa wameweka kambi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa lengo la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za afya na kuwafikia wananchi wengi zaidi wenye uhitaji wa matibabu ya kibingwa nchini.


No comments:
Post a Comment