
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limewakamata jumla ya watuhumiwa 45 wenye umri kati ya miaka 20 hadi 39 kwa tuhuma za kujihusisha na makosa mbalimbali ya uhalifu, ikiwa ni sehemu ya operesheni maalum iliyofanyika kuanzia Aprili 1 hadi 13, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP Gallus Hyera, amesema operesheni hiyo imelenga kuimarisha usalama wa raia na mali zao, pamoja na kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyojitokeza katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Kwa mujibu wa ACP Hyera, watuhumiwa wanane (08) walikamatwa kwa tuhuma za wizi wa miundombinu ya umeme, ambapo walikutwa na nyaya za shaba (copper wire), aluminium pamoja na earth wire zikiwa tayari zimeondolewa katika maeneo ya miradi ya umeme kuelekea uwanja wa ndege wa Msalato.
Aidha, watuhumiwa 21 wanaodaiwa kuwa ni vishandu walikamatwa kwa makosa ya unyang’anyi, uvunjaji na wizi nyakati za usiku. Katika operesheni hiyo, polisi walifanikiwa kukamata mali mbalimbali ikiwemo pikipiki tatu, televisheni sita, kamera za ulinzi (CCTV), redio, spika pamoja na vifaa vingine vinavyodaiwa kutumika katika uhalifu.
Katika hatua nyingine, watuhumiwa watano (05) walikamatwa kwa tuhuma za wizi wa mafuta ya dizeli lita 116 yaliyokuwa yakitumika katika miradi ya serikali, huku watuhumiwa wawili (02) wakikamatwa kwa tuhuma za utapeli kupitia kampuni ya Q-NET, wakidaiwa kuwahadaa zaidi ya watu 180 kwa ahadi za ajira na biashara.
ACP Hyera amesema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria.
Kwa upande wa usalama barabarani, amesema jumla ya madereva tisa (09) wa mabasi wamechukuliwa hatua za kisheria na kufungiwa leseni kutokana na makosa ya mwendo kasi, ulevi na uzembe uliosababisha ajali zenye madhara kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, polisi wameeleza kuwa mafanikio yamepatikana pia katika kesi za mahakamani ambapo watuhumiwa wanane (08) wamehukumiwa vifungo mbalimbali, ikiwemo kifungo cha maisha jela, miaka 30 kwa unyang’anyi wa kutumia silaha, pamoja na adhabu nyingine kulingana na makosa yao
Jeshi la polisi mkoa wa Dodoma limewataka wananchikuendelea kushirikuana na vyombo cya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu ili kusaidia kudhibiti vitendo hivyo na kuimarisha amani na usalama







No comments:
Post a Comment