
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, imepanga kuimarisha ukusanyaji, uhifadhi na usimamizi wa taarifa na nyaraka za kihistoria kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kidijitali ili kulinda historia ya taifa na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma.
Hayo yameelezwa Aprili 17, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani J. Kikwete, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Waziri Kikwete amesema katika mwaka huo wa fedha Serikali itakusanya taarifa, kumbukumbu, nyaraka na machapisho mbalimbali yanayohusu historia ya nchi kutoka taasisi za umma na watu binafsi, pamoja na kutambua na kuhifadhi kumbukumbu za Waasisi wa Taifa na Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu ikiwemo Keyword Filing System na e-File Management System katika Wizara, Idara na Mamlaka za Serikali za Mitaa, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na uwazi katika utendaji wa serikali.
Katika mapinduzi ya kidijitali, Idara hiyo itaimarisha Mfumo wa Usimamizi na Uhifadhi wa Kumbukumbu za Kielektroniki (Digital Records Management and Preservation System) ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kulinda nakala halisi za nyaraka za serikali.
Serikali pia imepanga kusaidia taasisi za umma kuandaa miongozo ya kuhifadhi na kuteketeza kumbukumbu, pamoja na kufanya tathmini ya kumbukumbu zilizopo katika vituo vya hifadhi ya nyaraka nchini.
Aidha, mafunzo na mikutano kazi itatolewa kwa watumishi na waratibu wa kumbukumbu ili kuwajengea uwezo kuhusu sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa nyaraka za serikali.
Katika kuongeza uelewa kwa umma, Serikali itatoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kwa maendeleo ya taifa.
Vilevile, Idara hiyo itafanya ukaguzi, uchambuzi na uhamishaji wa kumbukumbu tuli kutoka taasisi mbalimbali za umma na kuzihifadhi katika vituo maalum vya kitaifa.
Kwa mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imesema itaendelea kutoa ushauri wa kitaalam kwa taasisi za umma kuhusu usimamizi bora wa kumbukumbu ili kuhakikisha historia na taarifa muhimu za taifa zinahifadhiwa kwa usahihi na usalama wa muda mrefu.
Hatua hizo zinalenga kuimarisha utawala bora, uwazi na matumizi ya teknolojia katika kuhifadhi historia ya taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:
Post a Comment