SERIKALI YAUNGANISHA VYUO 33 VYA UALIMU NA MKONGO WA TAIFA KUPITIA MRADI WA TESP - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 10, 2026

SERIKALI YAUNGANISHA VYUO 33 VYA UALIMU NA MKONGO WA TAIFA KUPITIA MRADI WA TESP



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali imesema mradi wa Kuimarisha Mafunzo na Miundombinu katika Vyuo vya Ualimu (TESP) umefanikiwa kuunganisha vyuo 33 vya ualimu na Mkongo wa Taifa, hatua iliyorahisisha utoaji wa mafunzo kwa njia za kidijitali nchini.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kuhitimisha mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema hatua hiyo imeongeza ufanisi katika utoaji wa mafunzo na kupanua matumizi ya teknolojia katika vyuo vya ualimu.

Amesema kupitia mradi huo, vyuo hivyo vimeboreshwa kwa ujenzi wa maabara na maktaba, upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA, pamoja na kuongezwa kwa vitabu vya kujifunzia, hali iliyoinua ubora wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia nchini.

Akielezea Mradi TESP, Naibu Katibu Mkuu Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu,Prof Daniel Mushi, ameishukuru Serikali ya Canada kupitia taasisi ya Global Affairs Canada kwa ushirikiano na msaada wao uliochangia kuimarisha mifumo ya elimu ya ualimu nchini.

Ameeleza kuwa tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2017, kumekuwa na maboresho makubwa ikiwemo usambazaji wa zaidi ya vitabu laki moja tisini na sita katika vyuo 35 vya ualimu pamoja na kuunganishwa kwa taasisi hizo na mtandao wa maktaba za vyuo vikuu nchini.

Aidha, zaidi ya vifaa 1,400 vya TEHAMA vimesambazwa, hatua iliyosaidia kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, huku miundombinu kama maktaba na maabara ikijengwa na kukarabatiwa.

Katika hatua nyingine, zaidi ya wakufunzi 1,300 wamepatiwa mafunzo ya mbinu za kisasa za ufundishaji, elimu jumuishi pamoja na matumizi ya teknolojia, huku takribani walimu wanafunzi 73,000 wakihitimu katika kipindi cha mradi huo.

Prof. Mushi amesema mafanikio hayo ni uwekezaji mkubwa katika mustakabali wa elimu nchini, lakini akasisitiza kuwa ni muhimu sasa kuhakikisha yanaendelezwa kupitia ufadhili endelevu, uongozi imara wa taasisi na matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo.

Ametoa wito kwa washiriki wa kikao hicho kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza miradi hiyo, kupanua mafanikio yake katika taasisi nyingine na kuimarisha ushirikiano kati ya wizara, taasisi na wadau wa maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Tabora, Bi. Balbina Joseph, amesema kuwa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (Teachers Education Support Program – TESP), umeleta maboresho makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira, usawa wa kijinsia, ujumuishi na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

 Ameongeza kuwa wakufunzi, watumishi na bodi za vyuo wamepata mafunzo yaliyoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kabanga, Bw. Phonce Mashibe, amesema chuo hicho kimenufaika kwa kiasi kikubwa kupitia ujenzi upya wa miundombinu na uwekezaji katika mifumo ya nishati mbadala. Amefafanua kuwa matumizi ya biogas na nishati ya jua yamepunguza gharama za uendeshaji kwa kiasi kikubwa, zikishuka hadi asilimia 60.

Kwa upande wa wanafunzi, Marry Faustine Igulu, mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Bustani ngazi ya diploma, amesema kuwa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (Teachers Education Support Program – TESP),umeboresha kwa kiwango kikubwa mazingira ya kujifunzia, ikiwemo ujenzi wa maabara za sayansi, ukarabati wa mabweni, madarasa na maktaba.

 Ameongeza kuwa upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA umeongeza uwezo wa walimu tarajali kutumia teknolojia katika ufundishaji, hatua inayochangia kuinua ubora wa elimu nchini.








No comments:

Post a Comment