TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA COP12 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, April 20, 2026

TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA COP12


Na; Mwandishi Wetu
Dodoma


Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaotarajiwa kufanyika Oktoba 6 hadi 9 Oktoba 2026, Jijini Dar es Salaam, ukilenga kutoa fursa ya kujadili na kuimarisha mikakati ya pamoja ya usimamizi endelevu wa mazingira ya Bahari na Pwani.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda wakati akifungua Kikao cha Kwanza cha Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) na Mkutano wa 11 wa Bahari Yetu (the eleventh our ocean conference) uliofanyika Dodoma, Aprili 20, 2026.

“Kwa kuwa, Ofisi ya Makamu wa Rais ina jukumu la kuratibu, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Mkataba wa Nairobi nchini imeunda Kamati Kitaifa ya maandalizi ya mkutano wa COP12, inayojumuisha wadau kutoka Wizara, Taasisi na Idara za Serikali kwa lengo la kuhakikisha kuwa mkutano huo unafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu na nchi yetu inanufaika kikamilifu.

Balozi Luvanda, amesema Tanzania ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Nairobi kuhusu Hifadhi, Usimamizi na Uendelezaji wa Mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani ya Magharibi mwa Bahari ya Hindi.

Kila baada ya miaka miwili, Sekretarieti ya Mkataba huo huandaa Mkutano wa Nchi wanachama ambao hukutana na kujadili mafanikio na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Mkataba na Itifaki zake. Katika mkutano wake wa 11 uliofanyika Agosti 20 hadi 22, 2024 Jijini Antananarivo, nchini Madagascar, iliazimiwa Tanzania kuwa mwenyekiti wa Mkutano wa 12.

Pamoja na maandalizi ya mkutano wa COP-12, Tanzania imealikwa pia kushiriki katika Kongamano la 11 la Kimataifa la Bahari yetu “The Eleventh Our Ocean Conference” litakalofanyika Juni 16 hadi 18, 2026 katika Jiji la Mombasa nchini Kenya.

Kauli Mbiu ya Kongamano hili ni “Bahari yetu, Urithi wetu, Mustakabali wetu” (“Our Ocean, our heritage, our future”) ikiwa ni mara ya kwanza Kongamano hili kufanyika katika nchi za Afrika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Kitengo cha Maendeleo ya Uchumi wa Buluu na Uratibu, Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Magdalena Ngotolainyo amesema Mkutano wa COP12 utahusisha washiriki zaidi ya 500 ikiwemo viongozi wa nchi, wataalamu na wadau mbalimbali kutoka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi na wadau wengine.

“Ushiriki wetu katika mikutano hii, itafungua fursa za kiuchumi ikiwemo uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu, kuimarisha sekta za uvuvi na utalii, pamoja na kuanzisha miradi ya kikanda ya hifadhi ya mazingira ya Bahari na ukanda wa pwani.

Aidha, nchi itapata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu, pamoja na teknolojia mpya zitakazosaidia katika kuboresha Sera, Mipango, Mikakati na Programu bora za usimamizi wa rasilimali za bahari.

Naye, Mkufunzi Chuo cha Bahari, Mhandisi Gregory Mella amesema Mkutano wa COP12 pia umelenga katika kulinda vyanzo vya bahari na kuhakikisha watu wanapata rasilimali za bahari ikiwemo uvunaji wa mwani pamoja na uvuvi.

Ameongeza kuwa Tanzania imebahatika kuwa na zaidi ya kilomenta 1,400 za Ukanda wa Bahari hivyo wananchi wanauhusiano wa moja kwa moja na mazingira ya bahari, hivyo mikataba hii lengo lake ni kuhusisha wadau ili jamii inavyonufaika na rasilimali zinazopatikana baharini.

No comments:

Post a Comment