Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB), hatua inayotarajiwa kufungua fursa mpya za ufadhili kwa miradi ya kimkakati ya maendeleo, ikiwemo maji, nishati, usafiri, teknolojia ya habari na Mawasiliano pamoja na miundombinu ya kijani.
Hayo yamejiri wakati Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alipo ongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao na Rais wa Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB), Bi. Zou Jiayi, pembezoni mwa Mikutano ya Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Rais wa AIIB, Bi. Zou Jiayi, alisema kuwa Tanzania ni mdau muhimu katika Benki hiyo yenye Makao yake Makuu Beijing nchini China, na kwamba Benki yake imejipanga kuisaidia Serikali kutimiza malengo yaliyopangwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Aliyataja maeneo yenye kipaumbele kuwa ni pamoja na miundombinu ya usafiri wa Reli ya Kisasa, nishati, maji na mawasiliano ambapo kupitia uwekezaji huo, benki hiyo inalenga kuchochea maendeleo ya miundombinu, kupunguza umaskini, kuinua viwango vya maisha ya wananchi na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), aliikaribisha Benki hiyo kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa Mradi wa Reli iendayo kasi-SGR, ujenzi wa Bandari ya Mbegani Zanzibar, Miradi ya kukuza ajira kwa vijana katika sekta ya teknolojia na miradi mingine ambayo pande hizo mbili zitakubaliana.
Aidha, Mhe. Balozi Omar. alimweleza Rais huyo wa Benki ya AIIB umuhimu wa kuisaidia sekta binafsi kwa kuipatia mitaji ili iweze kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, ambapo sekta hiyo inatarajiwa kuchangia zaidi ya asilimia 70 ya malengo ya Tanzania kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050 kutoka makadirio ya ukuaji wa uchumi wa sasa wa dola za marekani takriban bilioni 100.
Tangu Tanzania iwe mwanachama asiye wa kikanda wa AIIB, Serikali imekuwa ikiitazama benki hiyo kama mshirika muhimu katika mkakati wa kupanua vyanzo vya fedha za maendeleo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia dira ya pamoja ya Benki hiyo ya “Infrastructure for Tomorrow”, inayolenga kujenga miundombinu ya kisasa na endelevu.





No comments:
Post a Comment