
Na Okuly Julius, OKULY BLOG , Dodoma
Tume ya Utumishi wa Umma (TUU) imeshughulikia jumla ya rufaa 60 na malalamiko 25 yaliyowasilishwa na watumishi wa umma katika mkutano wake wa tatu kwa mwaka wa fedha 2025/2026 uliofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 22,2026 jijini Dodoma , Kaimu Katibu wa Tume hiyo, John Mbisso, amesema mkutano huo ulifanyika kuanzia Machi 23 hadi Aprili 15, 2026 katika ukumbi wa UCSAF, eneo la Njedengwa, chini ya Mwenyekiti Jaji (Mst.) Hamisa Kalombola.
Amesema katika mkutano huo, Tume ilipitia, kujadili na kutoa maamuzi kwa jumla ya mashauri 85 yaliyowasilishwa, yakiwemo rufaa 60 na malalamiko 25 kutoka kwa watumishi wa umma.
Kwa mujibu wa Mbisso, makosa yaliyojitokeza zaidi katika rufaa hizo ni ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma, utoro kazini, uzembe uliosababisha hasara kwa mwajiri au Serikali, kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo pamoja na vitendo vya kuudhalilisha utumishi wa umma.
Aidha, amesema malalamiko mengi yalihusiana na kutopandishwa cheo, kutolipwa stahili, kuondolewa kazini bila kufuata sheria na taratibu, kutorekebishiwa cheo, kutobadilishiwa muundo wa utumishi baada ya kujiendeleza kielimu, pamoja na kusimamishwa kazi bila kuzingatia sheria.
Mbisso ameongeza kuwa baadhi ya walalamikaji walipewa nafasi ya kufika mbele ya Tume kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zao, hatua iliyochukuliwa kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.
Katika hatua nyingine, Tume iliita mamlaka mbili za nidhamu kufika mbele yake kutoa maelezo kuhusu ukiukwaji wa sheria na taratibu katika kushughulikia mashauri ya nidhamu ya watumishi walio chini yao.
Pia, Tume ilipitia taarifa tisa za utekelezaji wa majukumu yake na kutoa maelekezo mbalimbali kwa taasisi husika serikalini kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi.
Hata hivyo, Mbisso ametoa wito kwa watumishi wa umma kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi ili kuepuka hatua za kinidhamu au za kisheria.
Aidha, amewataka waajiri pamoja na mamlaka za ajira na nidhamu kuhakikisha wanazingatia sheria katika kushughulikia masuala ya watumishi, kuwasilisha kwa wakati vielelezo vya rufaa na malalamiko, pamoja na kutekeleza maagizo ya Tume kwa wakati.
“Tume itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sheria na kuhakikisha haki inatendeka kwa watumishi wa umma wote,” amesema Mbisso.

No comments:
Post a Comment