WATUMIAJI WA SIMU, INTANETI NA MIAMALA YA KIDIJITALI WAONGEZEKA KWA KASI NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 30, 2026

WATUMIAJI WA SIMU, INTANETI NA MIAMALA YA KIDIJITALI WAONGEZEKA KWA KASI NCHINI

 



Na Okuly Julius ,OKULY BLOG ,DODOMA


Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kuonesha ukuaji mkubwa nchini, huku ongezeko la watumiaji wa huduma mbalimbali za kidijitali likidhihirisha mafanikio ya uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali.


Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027. 


Alisema idadi ya laini za simu zilizosajiliwa imeongezeka kutoka milioni 90.4 Machi 2025 hadi kufikia milioni 111.9 Machi 2026, sawa na ongezeko la asilimia 23.8.


Alisema sambamba na hilo, matumizi ya intaneti yameendelea kupanuka ambapo watumiaji wameongezeka kutoka milioni 49.3 hadi milioni 58.9 katika kipindi hicho, sawa na ongezeko la asilimia 19.5.


Kwa upande wa huduma za fedha kwa njia ya simu, Waziri Kairuki alibainisha kuwa watumiaji wameongezeka kutoka milioni 66.5 hadi milioni 81.0, sawa na ongezeko la asilimia 21.8, hali inayoonesha kuimarika kwa matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali nchini.


“Takwimu hizi zinaonesha wazi jinsi wananchi wanavyozidi kuamini na kutumia huduma za TEHAMA katika maisha yao ya kila siku, hususan katika mawasiliano, biashara na huduma za kifedha,” alisema Waziri Kairuki.


Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alieleza kuwa idadi ya watoa huduma wa miundombinu ya mawasiliano imeongezeka kutoka 38 Machi 2025 hadi kufikia 52 Machi 2026, sawa na ongezeko la asilimia 36.8, jambo linaloashiria kuimarika kwa ushindani na uwekezaji katika sekta hiyo.


Aidha, watoa huduma za ziada (Application Services na Value-Added Services) wameongezeka kutoka 136 hadi 173 katika kipindi hicho, sawa na ongezeko la asilimia 27.2, hatua inayochochea ubunifu na upatikanaji wa huduma mbalimbali za kidijitali.


Waziri Kairuki alisisitiza kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwepo wa mifumo na mazingira wezeshi yaliyojengwa na Serikali chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye lengo la kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wengi zaidi mijini na vijijini.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji katika TEHAMA ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za kidijitali, sambamba na kukuza uchumi wa taifa unaotegemea teknolojia na ubunifu.

No comments:

Post a Comment