WAZIRI GWAJIMA AWAFUNDA MABINTI JASIRI UDSM - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, April 19, 2026

WAZIRI GWAJIMA AWAFUNDA MABINTI JASIRI UDSM


Na Mwandishi Wetu WMJWM- Dar Es Salaam


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka watoto wa kike kujipambanua katika kuhakikisha wanatumia muda wao kufanya mambo yatakayowasaidia katika ustawi wa maisha yao.

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo tarehe 18 Aprili, 2026 wakati akizindua Binti Jasiri UDSM inayoongozwa na kaulimbiu isemayo Weka Malengo, Piga Hatua Timiza Malengo.

Waziri Gwajima amesema jina la Binti Jasiri lina maana kubwa sana likiwakilisha ujasiri wa kusimama, kuota ndoto kubwa na kushinda changamoto hivyo katika ulimwengu wa leo, kunahitajika kuwa na mabinti ambao hawataogopa kushika nafasi za uongozi, kuanzisha biashara, wala kuchangia katika maamuzi makubwa ya kijamii na kiuchumi.

Ameeleza kuwa mpango huo umejengwa katika msingi imara unaoendana na dira ya maendeleo ya taifa yaani Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025, pamoja na malengo ya kimataifa ya maendeleo endelevu, hasa Elimu Bora (SDG 4) na Usawa wa Kijinsia (SDG 5).

“Binti Jasiri si tukio la siku moja bali ni mwanzo wa harakati endelevu na ni mwanzo wa kizazi kipya cha wanawake; Wenye maono, ujasiri na uwezo wa kubadilisha dunia.” Ameafafnua Waziri Dkt Gwajima.

Aidha amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado mabinti wengi wanakutana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mentorship, fursa za uongozi na rasilimali za kujiendeleza hivyo kupitia Binti Jasiri, inaunda mazingira yatakayowawezesha mabinti kujifunza uongozi, kuunganishwa na wale waliowatangulia na kujenga ujasiri wa kujitegemea na hatimaye kuwa suluhisho la changamoto za jamii.

“Nitoe wito kwa Mabinti wangu wapendwa, nataka muondoke hapa leo mkiwa na jambo moja moyoni ambalo ni uwezo, thamani kwani unaweza kufika mbali zaidi ya unavyodhani pia usiruhusu hofu, maneno ya watu au mazingira yakuzuie kwani Dunia inahitaji sauti yako, mchango wako na uongozi wako basi chukua nafasi Jitokeze na Jiamini.” Amesisitiza Waziri Gwajima

Pia amewataka wadau wote wanaotokea serikalini, sekta binafsi, taasisi na washirika kusisitiza kuwa kuwekeza kwa mwanamke kwani ni uwekezaji kwa taifa na kumuinua msichana mmoja ni kuinua familia, jamii na uchumi mzima hivyo amewahimiza kuendelea kuunga mkono mipango kama hiyo kutoa mentorship na kufungua milango ya fursa kwa vijana wa kike.

Kwa upande wake Makamu wa rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Joyce Juliasi Senkuli amesema Jukwaa hilo limeanzishwa kwa lengo la kumkomboa binti kifikra, kihisia, kielimu na kiuchumi, kwa kutambua kuwa bado wapo mabinti wengi wanaopitia changamoto mbalimbali katika safari ya maisha na elimu.

Naye Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Paulina Mabuga ameahidi kuwaunga mkono Mabinti hao ili waweze kufikia malengo yao katika kampeni walioianzisha ya kuwafanya Watoto wa kike kuinuka katika masuala mbalimbali katika jamii.


No comments:

Post a Comment