WAZIRI MKENDA: ELIMU YA UFUNDI NI UFUNGUO WA UCHUMI WA VIJANA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 29, 2026

WAZIRI MKENDA: ELIMU YA UFUNDI NI UFUNGUO WA UCHUMI WA VIJANA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema kuanzishwa kwa Wizara maalum ya maendeleo ya vijana ni uthibitisho wa namna Serikali inavyotambua umuhimu wa kundi hilo katika kukuza uchumi wa taifa.

Amesisitiza kuwa elimu ya ufundi kupitia VETA ni nyenzo muhimu ya kuwaandaa vijana kwa ujuzi unaowawezesha kuzalisha mali na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa.

Akizungumza Aprili 29, 2026 katika Mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, Prof. Mkenda amesema sekta ya elimu ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi, hivyo Wizara ina wajibu wa kuhakikisha mipango yote ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa sera ya elimu ya miaka 10 ya lazima pamoja na uimarishaji wa shule za sekondari na shule za amali unaendelea kufanyika kwa ushirikiano wa karibu na Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na sekta binafsi, hasa katika kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi na kuboresha miundombinu ya mafunzo kwa vifaa vya kisasa.

Katika kuhimiza uwajibikaji, Waziri Mkenda amewataka watumishi wa Wizara kuendeleza bidii na kuongeza kasi ya utendaji kazi, huku wakihakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu utekelezaji wa mipango na mafanikio ya Serikali katika sekta za elimu, sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo amesema Serikali inaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali watu na ajira kwa kuzingatia maono ya Samia Suluhu Hassan, hususan katika utekelezaji wa sheria na miongozo ya utumishi wa umma.

Amesema mkutano huo ni fursa muhimu kwa wajumbe kupitia mpango na bajeti ya Wizara, pamoja na kujadili masuala ya utawala bora, usimamizi wa rasilimali watu, na kuboresha afya na usalama mahali pa kazi.

Prof. Nombo amesisitiza kuwa mshikamano, ushirikiano na maadili ya kazi ni msingi wa kuongeza ufanisi na kuimarisha imani kwa umma, huku akiwataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo ili kufanikisha mageuzi ya sekta ya elimu.

Aidha, amewapongeza wajumbe wa Baraza hilo kwa mchango wao na kuwahimiza kuendeleza juhudi za kuimarisha mifumo ya usimamizi ndani ya Wizara kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.







No comments:

Post a Comment