Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Kanda ya Afrika, ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Kanda ya Afrika, Bw. Ronald Cafrine, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar Es Salaam.
Katika kikao hicho Mhe. Balozi Mussa Omar pamoja na Ujumbe huo wa Benki ya AfDB, walijadili masuala mbalimbali yanayolenga kuifanya nchi ya Tanzania kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza wakati wa kikao na Ujumbe huo, Mhe. Balozi Omar, aliipongeza benki hiyo kwa hatua mbalimbali za kuzikwamua kiuchumi nchi mbalimbali za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania.
‘’Mkurugennzi ningependa kuchukua fursa hii kuishukuru kwa dhati AfDB kwa ushirikiano na msaada wa masharti nafuu uliyotolewa kwa Tanzania chini ya ADF-16 ambao umekuwa muhimu katika kudumisha kasi katika mipango muhimu ya maendeleo’’ alisema Mhe. Balozi Omar.
Aliongeza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuwa inatambua mchango wa benki hiyo katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ya nishati pamoja na miundombinu mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Kanda ya Afrika Bw. Ronald Cafrine, alisema kuwa AfDB inatambua juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kujikwamua kiuchumi hivyo benki hiyo itaendelea kuiunga mkono Tanzania kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Naye Meneja wa Benki ya AfDB, Bi. Mary Manneko Monyau, alisema amevutiwa na mikakati mbalimbali na mipango ya maendeleo kupitia vipaumbele mbalimbali vilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa Tanzania, hivyo AfDB ipo tayari kuunga mkono juhudi hizo.
Benki ya Maendeleo ya Afrika hivi karibuni imeteua viongozi mbalimbali kwa upande wa Tanzania akiwemo Meneja wa Benki hiyo nchini Tanzania, Bi. Mary Manneko Monyau.






No comments:
Post a Comment