WAZIRI WA ULINZI NA JKT AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA ULINZI WA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, April 11, 2026

WAZIRI WA ULINZI NA JKT AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA ULINZI WA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb) tarehe 09 April, 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mheshimiwa Guy Kabombo Muadiamvita aliyefanya ziara ya kikazi nchini Tanzania.

Mazungumzo hayo ya Kikazi baina ya Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yalifanyika katika Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Kikombo jijini Dodoma, yalilenga kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu na kihistoria baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika Diplomasia ya Ulinzi.

Katika kikao hicho, Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt Rhimo Nyansaho amemhakikishia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kongo,utayari wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ulinzi na JKT, kushirikiana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika nyanja mbalimbali za Ulinzi, hususani katika Ubadilishanaji wa wataalamu, Mafunzo, pamoja na ushirikiano dhidi ya changamoto za kiusalama kama, Uhalifu wa mtandaoni na vita dhidi ya ugaidi.

Dkt Rhimo Nyansaho amemueleza Mgeni wake Naibu Waziri Mkuu wa Kongo Mhe, Guy Kabombo kuwa, ziara yake nchini Tanzania, ni ushahidi wa uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili huku ikionyesha umuhimu mkubwa katika kuendelea kudumisha na kuimarisha maelewano, ushirikiano na urafiki kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuongeza kuwa kwa miaka mingi kumekuwa na majadiliano ya wazi yenye nia ya kujenga na kuweka misingi ya ushirikiano madhubuti kati ya Tanzania na Kongo.

“Nina Imani kuwa kupitia ushirikiano na uhusiano wetu sio kwamba tutakabiliana na changamoto zinazotukabili kwa pamoja, pia tutanufaika na fursa zilizopo mbele yetu ili kuchochea ukuaji na ustawi wa pamoja”, alisema Dkt. Rhimo Nyansaho.

Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt Rhimo Nyansaho ameongeza na kumueleza Mgeni wake, Mhe Guy Kabombo Muadiamvita, kuwa serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zina nafasi na fursa kubwa ya kunufaika na ushirikiano wa kibiashara na uchumi kwa pande zote mbili hususan katika usafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Dar-es-salaam na njia nyinginezo za kiuchumi na hivyo kuboresha ustawi na maendeleo ya wananchi wa Tanzania na Kongo. Waziri Rhimo Nyansaho akamuhakikishia Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, utayari wa Tanzania kuiona Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inastawi na kuwa imara kiuchumi na kiusalama.













No comments:

Post a Comment