BAJETI YA MALIASILI NA UTALII 2026/2027 YAWEKA WAZI VIPAUMBELE VYAKE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 15, 2026

BAJETI YA MALIASILI NA UTALII 2026/2027 YAWEKA WAZI VIPAUMBELE VYAKE



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Wizara ya Maliasili na Utalii imetaja vipaumbele tisa vitakavyoongoza utekelezaji wa bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, vikilenga kuimarisha uhifadhi wa rasilimali, kukuza utalii, kuboresha miundombinu pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta hiyo.

Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma Mei 15, 2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali itaendelea kuweka mkazo katika uhifadhi, ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori, misitu, nyuki na malikale ili kuhakikisha sekta hiyo inachangia zaidi ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Dkt. Kijaji amesema kipaumbele kingine ni kuimarisha miundombinu wezeshi katika maeneo ya utalii na hifadhi ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, mawasiliano pamoja na huduma za kijamii kwa lengo la kuboresha huduma kwa watalii na kuongeza ushindani wa Tanzania kimataifa.

Aidha, Wizara itaendelea kuimarisha utangazaji wa utalii ndani na nje ya nchi kupitia masoko mbalimbali ya kimkakati ikiwemo Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati huku ikitumia fursa za matukio makubwa ya kimataifa kama Africa Cup of Nations 2027, mikutano ya kimataifa pamoja na mashindano ya ulimbwende duniani kuitangaza Tanzania.

Amesema Serikali pia imeweka mkazo katika kuendeleza na kuboresha mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo utalii wa meli, mikutano na matukio ya biashara (MICE), sambamba na kutambua na kusajili mazao mapya ya utalii.

Katika sekta ya misitu na nyuki, Waziri huyo alisema Serikali itaendelea kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao pamoja na kupanua masoko ya bidhaa hizo ndani na nje ya nchi.

Dkt. Kijaji amebainisha kuwa matumizi ya teknolojia za kisasa nayo yatapewa kipaumbele katika usimamizi wa rasilimali, ulinzi, ufuatiliaji wa shughuli mbalimbali, ukusanyaji wa mapato pamoja na utangazaji wa vivutio vya utalii.

Vipaumbele vingine vilivyotajwa ni pamoja na kuimarisha utafiti, ubunifu na maendeleo ya rasilimali watu, kufanya mapitio ya sera, sheria, kanuni na miongozo ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia pamoja na kuboresha mazingira ya kazi, mifumo ya usimamizi wa utendaji na uwajibikaji.


Ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele hivyo, Ashatu Kijaji ameliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha Shilingi bilioni 334 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika mwaka wa fedha 2026/2027.

No comments:

Post a Comment