DC MODEST AZITAKA TAASISI ARUSHA KUTUMIA NISHATI SAFI KUPIKIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, May 9, 2026

DC MODEST AZITAKA TAASISI ARUSHA KUTUMIA NISHATI SAFI KUPIKIA


Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Modest, amezitaka taasisi zote zinazohudumia zaidi ya watu 100 kwa Mkoa wa Arusha kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya za wananchi na mazingira.

Mhe.Modest, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, katika hafla ya uzinduzi wa chapa mpya ya LOTI Gesi, amesema hatua hiyo inalenga kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuhakikisha huduma hiyo inawafikia Watanzania wote.

Amesema utekelezaji wa agizo la Serikali linalozitaka taasisi zinazolisha zaidi ya watu 100 kutumia nishati safi ya kupikia ni muhimu katika kulinda afya za wananchi na mazingira, na kuunga mkono jitihada za Taifa za kuhifadhi mazingira na kupunguza athari za matumizi ya nishati zisizo salama.

Aidha, ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, unaolenga kuhakikisha taasisi za umma, ikiwamo shule, zinatumia teknolojia salama, bora na rafiki kwa mazingira katika shughuli za upishi.

Mhe. Modest amesema Wilaya ya Arusha inaendelea kutekeleza kwa mafanikio agizo hilo la Serikali, huku akizitaka taasisi ambazo bado zinatumia nishati zisizo safi kuhakikisha zinahamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Pia ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza na kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia, ili kuongeza uelewa na kuhamasisha matumizi yake nchini.

No comments:

Post a Comment