Dkt. William Ruto Aipongeza NSSF Tanzania Kwa Uwekezaji wa Dola zaidi ya Milioni 51 Nairobi - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 6, 2026

Dkt. William Ruto Aipongeza NSSF Tanzania Kwa Uwekezaji wa Dola zaidi ya Milioni 51 Nairobi

Rais wa Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto, ameusifu uwekezaji wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wa Tanzania unaoendelea jijini Nairobi, akisema ni mfano bora wa matumizi sahihi ya akiba za wanachama katika kukuza uchumi na maendeleo ya kikanda.

Akizungumza Mei 5, 2026 wakati akihutubia Bunge jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Ruto alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Tanzania, Bw. Masha Mshomba, kwa usimamizi thabiti wa uwekezaji huo, akibainisha kuwa unaonesha namna bora ya kugeuza akiba za wanachama kuwa miradi yenye tija.

Alisema mradi huo uliopo eneo la Upper Hill, jijini Nairobi, unahusisha ujenzi wa majengo pacha yenye ghorofa 22, unaogharimu takribani dola za Marekani zaidi ya Milioni 51. Mradi huo unatekelezwa kwa kutumia akiba za wanachama wa NSSF Tanzania na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili.

Mhe. Dkt. Ruto alieleza kuwa uwekezaji huo ni somo muhimu kwa Kenya na mataifa mengine ya Afrika Mashariki kuhusu umuhimu wa kukuza utamaduni wa akiba na uwekezaji kwa maendeleo ya muda mrefu.

“Uwekezaji ni zao la akiba. Huwezi kuwekeza kama huna akiba,” alisisitiza Dkt. Ruto, akihimiza wananchi na taasisi kuzingatia nidhamu ya kuchangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii kwa mustakabali wa baadaye.

Aidha, alibainisha kuwa nchini Kenya wamefanya maboresho ya mfumo wa hifadhi ya jamii mwaka 2023 baada ya kujifunza kutoka mifumo bora ikiwemo ya Tanzania.

Alieleza kuwa mfumo huo unahitaji mwajiri na mwajiriwa kuchangia kwa pamoja hadi asilimia 20 ya mapato ili kuimarisha usalama wa kifedha kwa wafanyakazi wanapostaafu.

Mhe. Dkt. Ruto alisisitiza kuwa utamaduni wa kujiwekea akiba unapaswa kuendelezwa ndani ya jamii, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kujenga mifumo imara ya hifadhi ya jamii.

Rais Dkt. Ruto pia alisifu mafanikio ya Tanzania katika sekta ya hifadhi ya jamii, akieleza kuwa Kenya inaendelea kujifunza na kuchukua mifano bora kutoka kwa majirani zake.

Katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, alisema anajivunia uhusiano mzuri uliopo kati ya Kenya na Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa huu ni wakati muhimu katika historia ya mataifa hayo mawili.

Akihitimisha, Dkt. Ruto amesema kuwa kwa sasa kuna hatua kubwa ya kihistoria katika uhusiano wa Kenya na Tanzania, akieleza furaha yake kwa ushirikiano wa karibu kati yake na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema viongozi hao wanafanya kazi kwa pamoja kuwaleta karibu wananchi wa Afrika Mashariki na kuondoa changamoto zilizodumaza maendeleo kwa muda mrefu.

Kauli hiyo inaakisi mwelekeo wa mataifa ya Afrika Mashariki katika kutumia rasilimali zao za ndani kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Rais Dkt. William Ruto anahitimisha ziara rasmi ya siku mbili nchini Tanzania, iliyoanza Mei 4 hadi 5, 2026.













No comments:

Post a Comment