Na Okuly Julius, OKULY BLOG
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imetangaza kuwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia kwa mwaka 2026 yatafanyika rasmi Juni 30, 2026 kwa kuunganishwa na maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, ikiwa ni mkakati wa kuunganisha nguvu za wadau katika kuhimiza malezi bora ya watoto na ustawi wa familia nchini.
Akitoa taarifa hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima amesema kuwa Tanzania imekuwa ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia kila mwaka tarehe 15 Mei kupitia shughuli mbalimbali zinazolenga kuimarisha taasisi ya familia na ustawi wa jamii.
Amesema kwa mwaka huu Wizara pamoja na wadau wameamua kuyaunganisha maadhimisho hayo na Siku ya Mtoto wa Afrika ili kutoa sauti kubwa zaidi kuhusu umuhimu wa familia katika malezi na makuzi ya watoto.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na kaulimbiu isemayo, “Mtoto ni Malezi; Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara.” Kaulimbiu hiyo inalenga kusisitiza umuhimu wa malezi bora ya watoto kuanzia kipindi cha ujauzito hadi wanapofikisha umri wa miaka 18.
Dkt. Gwajima amesema jamii inapaswa kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira yenye maadili mema, upendo, ulinzi na usalama ili kuwajengea msingi imara wa maisha yao ya baadaye.
“Maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ya taifa letu yatategemea namna watoto wanavyolelewa na kukuzwa kwa kuzingatia misingi bora ya maadili pamoja na mila na desturi njema za Kitanzania,” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa uwekezaji katika malezi ya watoto ni hatua muhimu ya kujenga familia bora na taifa lenye nguvu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Katika taarifa hiyo, Waziri huyo ametangaza kuwa kuanzia Mei 15, 2026 wananchi wote wanapaswa kuanza kutafakari nafasi ya familia katika malezi na makuzi ya watoto pamoja na kufuatilia elimu mbalimbali kupitia vyombo vya habari kuhusu umuhimu wa familia katika maendeleo ya taifa.
Pia amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu mwenendo wa maadhimisho hayo kuelekea kilele chake kitakachofanyika Juni 30, 2026.


No comments:
Post a Comment