SERIKALI YAIMARISHA AFYA YA MIMEA KUHAKIKISHA USALAMA WA CHAKULA NA LISHE NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 13, 2026

SERIKALI YAIMARISHA AFYA YA MIMEA KUHAKIKISHA USALAMA WA CHAKULA NA LISHE NCHINI



Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha afya ya mimea nchini kama sehemu ya kuhakikisha usalama wa chakula na lishe kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania itaendelea kuimarisha huduma za afya ya mimea ili kuongeza tija katika Sekta ya Kilimo na kufikia malengo ya Agenda 10/30 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050
Kauli hiyo aliitoa wakati akimwakilisha Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea yaliyofanyika jijini Dodoma tarehe 12 Mei 2026.

Katika hotuba yake, Mhe. Silinde alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuimarisha huduma za kidijiti nchini ambazo zimeendelea kusaidia maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo kilimo.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi katika kulinda bayoanuai ya mimea ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uzalishaji endelevu wa chakula na lishe bora kwa wananchi wote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania, Prof. Joseph Ndunguru amesema Tanzania imefikia kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa asilimia 130 katika mwaka 2024/2025, huku uzalishaji wa chakula ukifikia tani 23,783,128.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada mbalimbali za kudhibiti visumbufu vya mazao ikiwemo operesheni ya kudhibiti baa la panya katika mikoa 19, ambapo ekari 408,109 za mazao ziliokolewa na zaidi ya wakulima 66,511 kunufaika.

Prof. Ndunguru ameongeza kuwa mamlaka hiyo pia imefanikiwa kudhibiti zaidi ya ndege waharibifu milioni 231 aina ya kwelea kwelea waliokuwa wakivamia mashamba ya mpunga, mtama na uwele, hatua iliyookoa takribani tani 1,611,000 za mazao.

Vilevile, katika kukabiliana na viwavijeshi, TPHPA ilifanya operesheni za udhibiti katika hekta 219,411 kwenye wilaya 49 nchini na kuokoa zaidi ya tani 529,347 za mazao ya mahindi na mtama.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ilikuwa “Ulinzi wa Bayoanuai ya Mimea kwa Usalama wa Chakula na Lishe.”




No comments:

Post a Comment