
Na Edward Winchislaus, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali imeendelea kuimarisha jitihada za kuhakikisha kuwa sera, mipango na bajeti zinakuwa chombo madhubuti cha kuleta usawa, ustawi na maendeleo kwa Watanzania wote bila kujali jinsia.
Hayo yamebainishwa leo Mei 05,2026 jijini Dodoma na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, wakati akifungua semina kwa wabunge kuhusu uingizaji wa masuala ya kijinsia katika mipango na bajeti.

Amesema kuwa mkutano huo haujalenga mazungumzo ya kawaida, bali umejikita katika kujenga msingi imara utakaohakikisha kuwa kila kundi katika jamii linanufaika na rasilimali za taifa kwa usawa.
“Kukutana hapa leo si kwa ajili ya mazungumzo ya kawaida, bali ni kujenga misingi imara ya kuhakikisha sera, mipango na bajeti zinakuwa chombo cha usawa na maendeleo kwa wote,” amesema Dkt. Gwajima.
Katika kuendeleza uchumi wa taifa, Tanzania imejipanga kutekeleza Dira ya Maendeleo ya 2050 pamoja na mikakati ya kitaifa ya kupunguza umasikini. Hata hivyo, imeelezwa kuwa mafanikio ya malengo hayo yanategemea ushiriki sawa wa wanawake, wanaume na vijana wa jinsia zote katika kupanga na kunufaika na rasilimali zilizopo.
Aidha, imeelezwa kuwa wanawake wamekuwa wakichangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya taifa, hususan katika sekta ya kilimo pamoja na mchango huo mkubwa, bado hawajatambuliwa ipasavyo katika takwimu za kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na mifumo ya upangaji bajeti isiyozingatia tofauti za kijinsia.
Takwimu zimeonesha kuwa zaidi ya asilimia 65 ya wanawake vijijini wamejishughulisha na kilimo, lakini wameendelea kukumbwa na changamoto ya ukosefu wa mikopo, pembejeo bora na masoko ya uhakika. Hali hii imeendelea kuathiri uwezo wao wa kuinua uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.
Serikali imeendelea kusisitiza kuwa bajeti inayozingatia jinsia imekuwa si tu nyenzo ya usawa bali pia kichocheo cha ukuaji wa uchumi. “Bajeti inayozingatia jinsia siyo nyenzo ya usawa pekee, bali ni chombo muhimu cha kuongeza tija ya uchumi wa taifa,” ameongeza.
Uzoefu kutoka nchi kama Rwanda na Uganda umeonesha kuwa uwekezaji katika sera na bajeti zenye mrengo wa kijinsia umeleta matokeo chanya katika uwakilishi wa wanawake na utoaji wa huduma muhimu za kijamii.
Kupitia semina hiyo, wabunge wamepata fursa ya kujifunza mbinu bora za kuchambua bajeti kwa mtazamo wa kijinsia, kuishauri serikali na kufuatilia utekelezaji wake.












No comments:
Post a Comment