Naibu Kamishna wa Polisi, DCP Renata Mzinga amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii katika kudumisha amani na utulivu nchini.
Ameyasema hayo tarehe 02 Mei, 2026 alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Familia ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga yaliyofanyika katika viwanja vya Usagara, Jijini Tanga.
DCP Mzinga alieleza kuwa maadhimisho hayo ni jukwaa muhimu la kuimarisha mshikamano, mahusiano mema na mawasiliano kati ya askari na wananchi, hali inayochangia kuongezeka kwa ufanisi wa ulinzi na usalama.
Aidha, alihimiza askari kuendelea kufanya kazi kwa weledi, utii na kutenda haki, sambamba na kuimarisha ushirikiano na jamii ili kudumisha amani iliyopo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi alitoa shukrani kwa wananchi na wadau mbalimbali kwa kushiriki katika maadhimisho hayo na kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia falsafa ya Polisi Jamii na ulinzi shirikishi.
Maadhimisho hayo yalipambwa na michezo na burudani mbalimbali ikiwemo kuvuta kamba na kukimbiza kuku, ambapo askari walishiriki pamoja na familia zao na wananchi katika hali ya furaha na mshikamano.












No comments:
Post a Comment