Na Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Serikali inaendelea
kuwekeza katika uendelezaji wa rasilimali za maji kwa kujenga miundombinu himilivu
itakayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ukame na
mafuriko.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi
ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Aweso amesema juhudi hizo
zinahusisha ujenzi wa mabwawa na miradi ya uvunaji wa maji ya mvua ili
kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma ya maji nchini.
Ameeleza kuwa ujenzi wa Bwawa la Kidunda
unaendelea kwa lengo la kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam
pamoja na Mikoa ya Pwani na Morogoro, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia
47.02, ukiwa na gharama ya shilingi bilioni 329.47.
Aidha, Serikali imefanikiwa kumpata
mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Farkwa, litakalosaidia kuboresha
huduma ya maji katika Jiji la Dodoma na Wilaya za Chamwino, Bahi na Chemba, kwa
gharama ya shilingi bilioni 312.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amesema
Serikali imekamilisha ujenzi wa mabwawa 11 katika maeneo mbalimbali nchini,
hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na
shughuli za kiuchumi.
Kuhusu ubora wa maji, Aweso amesema Serikali
imeendelea kuimarisha huduma hiyo kupitia ufuatiliaji wa vyanzo vya maji,
uhakiki wa maji ya kunywa, udhibiti wa majitaka pamoja na kuendeleza uwezo wa
maabara.
Amefafanua kuwa katika mwaka 2025/26, jumla
ya vyanzo 424 vilifanyiwa uchunguzi, huku skimu 690 za maji vijijini na
mitandao 351 ya maji mijini zikihakikiwa ubora wake. Pia, maabara 17
zimejengewa uwezo na saba kati yake zimeendelea kudumisha ithibati ya
kimataifa.
Kwa upande wa udhibiti wa majitaka, amesema
sampuli 123 kutoka mifumo 84 zilichunguzwa ili kuhakikisha maji yanayosafishwa
yanakidhi viwango vinavyokubalika kabla ya kurejeshwa kwenye mazingira.
Aweso amesisitiza kuwa uhakiki wa ubora wa
maji kabla ya matumizi ni muhimu katika kulinda afya za wananchi na mazingira,
akitoa wito kwa wadau wote kuhakikisha wanazingatia viwango vinavyotakiwa.
“Ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha maji
yanayotumika ni salama. Vilevile, viwanda na taasisi zinazozalisha majitaka
lazima yahakikishe yanatibiwa ipasavyo kabla ya kurejeshwa kwenye mazingira,”
amesema Aweso.


No comments:
Post a Comment