WIZARA YA MAJI KUDHIBITI UPOTEVU WA MAJI KWA TEKNOLOJIA ZA KISASA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 5, 2026

WIZARA YA MAJI KUDHIBITI UPOTEVU WA MAJI KWA TEKNOLOJIA ZA KISASA


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Serikali imepanga kuongeza kasi ya kudhibiti upotevu wa maji kwa kutumia teknolojia za kisasa pamoja na kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya maji nchini katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Akizungumza wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji, Aweso amesema hatua hiyo inalenga kuboresha ufanisi wa huduma za maji na kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa uhakika.

Amesema katika kipindi hicho, jumla ya vyanzo vya maji 2,200 vitafuatiliwa na kuhakikiwa ubora wake, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji na usafi wa mazingira.

Aidha, Wizara imepanga kutambua na kuweka mipaka katika vyanzo 45 vya maji na kuvitangaza kuwa maeneo tengefu, pamoja na kukarabati vituo 100 vya ufuatiliaji wa mwenendo wa maji katika mito na vituo 50 vya uchunguzi wa maji chini ya ardhi.

Katika kuongeza upatikanaji wa maji, Wizara itajenga na kukarabati mabwawa 35, kufanya usanifu wa mabwawa mapya 34, pamoja na kuchimba visima virefu 300 katika maeneo yenye uhaba wa maji, huku ikiendelea na miradi ya uhamishaji maji kati ya mabonde.

Kuhusu ubora wa maji, Aweso amesema mifumo 8,245 ya maji vijijini na mijini pamoja na mifumo 150 ya majitaka itahakikiwa, sambamba na kuimarisha maabara 17 za upimaji wa ubora wa maji.

Kwa upande wa vijijini, Wizara itatekeleza miradi 992 ya maji na kuanzisha miradi katika vijiji 314 ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo, huku Vyombo vya Watumiaji Maji (CBWSOs) 918 vikiendelea kuimarishwa.
Katika maeneo ya mijini, Wizara itaendelea na miradi 222 ya maji pamoja na miradi ya Gridi ya Taifa ya Maji, ikiwemo miradi ya Kiwira, Ruvuma na Rufiji, pamoja na kuendeleza Bwawa la Farkwa jijini Dodoma.

Aidha, miradi 26 ya usafi wa mazingira itaendelea kutekelezwa ili kulinda afya za wananchi na mazingira.

Aweso amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutumia teknolojia na mifumo ya TEHAMA kupunguza upotevu wa maji, huku ikichukua hatua za kisheria kwa waharibifu wa miundombinu, ili kuhakikisha huduma za maji zinakuwa bora, salama na endelevu nchini.

No comments:

Post a Comment