![]() |
| Naibu Waziri wa Wizara ya Maji Maryprisca Mahundi akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 12,2022 kuhusu Vipaumbele vya Wizara hiyo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 jijini Dodoma. |
Na Okuly Julius Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Maji imepanga kutekeleza jumla ya miradi 1029 ya maji Vijijini ambapo miradi 648 ni miradi inayoendelea kutekelezwa na miradi 381 ni mipya.
Utekelezaji wa miradi hiyo unategemewa kupunguza adha ya upatikanaji wa maji kwa wananchi, kuongeza ajira na kupunguza gharama za matibabu kutokana na magonjwa yanayohusiana na maji.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Agosti 12,2022 wakati akielezea kuhusu Vipaumbele vya Wizara hiyo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Naibu Waziri wa Wizara ya Maji Maryprisca Mahundi amesema kuwa wanataka kuhakikisha kuwa upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi waishio vijijini inafikia zaidi ya asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.
Mhe.Mahundi amebainisha kuwa kumekuwa na milipuko ya magonjwa yanayoibuka katika baadhi ya maeneo hasa vijijini inayosababishwa na matumizi ya maji ambayo sio salama hivyo wizara imedhamiria kuhakikisha kuwa huduma ya majisafi na salama inapatikana kuondokana na matatozo hayo.
"Magonjwa mengine yawezekana ni matumizi ya maji ambayo sio salama sasa kwa serikali hii ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais Samia tumejizatiti kwenda kutibu kabisa tatizo hilo kwa kuwapelekea wanavijiji maji safi na salama na miradi hii ikikamilika huduma ya majisafi na salama itakuwafikia wananchi"Amesema Mhe.Mahundi
Kwa upande wa uboreshaji na upatikanaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini Mhe.Mahundi amesema kuwa Wizara imepanga kutekeleza jumla ya miradi 175 yenye kulenga kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi waishio mijini.
"utekelezaji huo ni sehemu ya kufikia zaidi ya asilimia 95 ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya mijini ifikapo mwaka 2025,"Ameeleza Mhe.Mahundi
Na kuongeza kuwa "Kwa upande wa kuboresha huduma ya usafi wa mazingira nchini Wizara itatekeleza miradi ya usafi wa mazingira katika miji 10, pia itaendelea na utekelezaji wa miradi ya usafi wa mazingira katika miji ya Babati, Dodoma, Mbeya, Iringa na Dar es Salaam"Mhe.Mahundi
Pia Mhe.Mahundi amebainisha kuwa usimamizi wa ubora wa maji ni mojawapo ya masuala muhimu katika maendeleo ya taifa, kulinda afya ya jamii, mazingira na vyanzo vya maji.
Amesema kuwa Wizara kupitia maabara 17 za ubora wa maji nchini itaendelea kuhakiki na kufuatilia ubora wa maji katika vyanzo vya maji na mitandao ya kusambaza maji mijini na vijijini kwa lengo la kutoa maamuzi sahihi kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Ikumbukwe kuwa Wizara ya Maji katika mwaka fedha 2022/23 imeidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni 709.3 kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya wizara hiyo ikiwemo matumizi ya kawaida,kulipa mishahara ya watumishi wa Wizara,RUWASA na Chuo cha maji pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo.


No comments:
Post a Comment