
Tukio la kihistoria limefanyika leo tarehe 25 April, 2025, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi imezindua rasmi safari za ndege ya Air Tanzania kati ya Dar es Salaam, Tanzania na Kinshasa, DRC katika hafla iliyofanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N'djili ulioko Kinshasa Nchini DRC na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wawekezaji, Mabalozi pamoja na wanahabari.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mgeni rasmi Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Prof Makame Mbarawa amewashukuru Viongozi Wakuu wa Nchi zote mbili kwa maono haya ambayo yameandika historia mpya katika mashirikiano
Amesema kuwa uzinduzi huo ni hatua kubwa katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na DRC na ni ishara ya uanzishwaji wa dira mpya ya ushirikiano wa kikanda

"Uzinduzi huu ni zaidi ya tukio la usafiri, ni ishara ya ushirikiano mpya utakaofungua fursa nyingi za biashara, kukuza utalii na ajira kwa wananchi wa nchi zote mbili " amesisitiza Mbarawa
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Waziri ameipongeza Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) kwa kufanikisha safari hii mpya, na kuhimiza umuhimu wa kutoa huduma bora kwa abiria na kuhakikisha usalama wa hali ya juu.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi ya DRC Mhe Paul Djunga kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi wa Nchi hiyo na Naibu Waziri Mkuu Mhe Jean Pierre Bemba ameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, akisema kuwa ni mwanzo mpya wa ushirikiano thabiti baina ya mataifa hayo mawili jirani na ni kiashiria cha safari ya matumaini, maendeleo na mshikamano wa bara Afrika
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mha Peter Ulanga amesema safari hizi zitakuwa zikifanyika katika siku nne za wiki ambazo ni jumapili, jumatatu, jumatano na ijumaa na itatumia masaa matatu na dk 20 ambapo itapunguza sana mda wa safari kati ya kinshasha, Kongo na Dar es salaam, Tanzania na kufungua fursa za kiuchumi kikanda
Amesema mbali na maeneo mengine ambayo ATCL inaenda, Kinshasa utakuwa ni mji wa pili ambao inafanya safari zake mwingine ni Lubumbashi na kampuni itaendelea kutanua wigo ili kufikia vituo vingi zaidi vya Kimataifa.












No comments:
Post a Comment