
Na Okuly Julius _ DODOMA
Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema katika kipindi cha miaka minne (2020/21 - 2024/25), Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanikiwa kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama nchini kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati.
Aweso ametoaka kauli hiyo leo Mei 8,2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/26 ,
Ambapo ameeleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya sera madhubuti na usimamizi thabiti wa utekelezaji wa miradi ya maji, ukiwemo upitishaji wa Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 Toleo la 2025.
"Sera hii mpya inalenga kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za maji, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha usafi wa mazingira vijijini, na kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wa miradi ya maji," amesema Aweso
Kwa upande wa vijijini, Waziri Aweso amesema jumla ya miradi 1,965 ya usambazaji maji imekamilika na kuhudumia vijiji 5,521, na hivyo kufanya idadi ya vijiji vilivyofikiwa na huduma ya maji kufikia 10,779 kati ya vijiji 12,318 vilivyopo nchini.
Hili limeongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kutoka asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asilimia 83 kufikia Desemba 2024.
"Katika maeneo ya mijini, miradi 366 ya usambazaji maji imekamilika na imewanufaisha zaidi ya wakazi milioni 6.2, hali iliyoongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka wastani wa asilimia 84 hadi 91.6.,"ameeleza Aweso
Amesema mafanikio hayo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuboresha maisha ya wananchi kupitia huduma bora za kijamii, hasa maji safi ambayo ni msingi wa maendeleo ya afya, elimu, na uchumi wa wananchi.
No comments:
Post a Comment