DKT. BITEKO AWATAKA MAAFISA MAENDELEO JAMII KUIPA THAMANI TAALUMA YAO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 7, 2025

DKT. BITEKO AWATAKA MAAFISA MAENDELEO JAMII KUIPA THAMANI TAALUMA YAO


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kote nchini kuhakikisha wanashirikishwa kikamilifu katika mipango ya maendeleo kuanzia ngazi za halmashauri ili kuchochea maendeleo jumuishi na endelevu kwa manufaa ya Taifa.

Akizungumza katika Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii nchini uliofanyika jijini Dodoma, Dkt. Biteko amesema ni muhimu kwa Maafisa hao kujitambulisha na kuwa sehemu ya utekelezaji wa mipango, badala ya kusubiri kuitwa wakati wa changamoto.


 “Mahali popote ulipo, ni muhimu kila mtu ajue upo; usisubiri uambiwe au litokee tatizo ndio waseme nani anaweza. Wapeni sababu wakuu wenu kuwatafuta, kupitia chama chenu, furukuteni kwenye halmashauri zenu,” amesema.

Ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametambua mchango wa kada hiyo kwa kuanzisha Wizara maalum ya Maendeleo ya Jamii, sambamba na kuongeza ajira kwa zaidi ya asilimia 50 kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.


Dkt. Biteko ametoa wito kwa taasisi mbalimbali za Serikali, mashirika, wakala, na tume kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kupanga na kutekeleza maendeleo, akisisitiza kuwa wao ni wakala wa maendeleo na hawapaswi kuachwa nje.

Amesisitiza kuwa licha ya majukumu yao kama wasajili wa wafanyabiashara wadogo na NGOs, maafisa hao hawapaswi kutumiwa tu wakati wa changamoto za mikopo, bali washirikishwe kikamilifu katika kupanga maendeleo.

Akitaja juhudi za Serikali, Dkt. Biteko amesema kuwa katika miaka ya fedha 2022/23 hadi 2024/25, jumla ya wataalamu 1,500 wa maendeleo ya jamii wameajiriwa ili kuimarisha utoaji huduma katika ngazi ya msingi. Pia, ameeleza kuanzishwa kwa Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi (2022/23 - 2025/26) na Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM).


Aidha, ameeleza kuwa Serikali imezindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034), unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo 2034. Kwa mwaka 2024/25, Serikali imetoa ruzuku kwa mitungi ya gesi kwa nusu ya bei katika maeneo ya vijijini na mijini.

Dkt. Biteko amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kusambaza umeme na kuhamasisha matumizi ya nishati safi. Pia, amewataka kuendelea kuibua fursa za kiuchumi, kutoa elimu na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika fursa mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), Mikopo ya Asilimia 10 ya Mapato ya Halmashauri, na mikopo ya wajasiriamali wadogo.

Amesisitiza kuwa maafisa hao, kama wasajili wasaidizi wa NGOs, ni viunganishi muhimu kati ya Serikali na mashirika hayo na wanapaswa kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa.


Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Doroth Gwajima, amesema mkutano huo umehudhuriwa na wadau 1,238 kutoka sekta ya umma na binafsi.

Amesema Maafisa Maendeleo ya Jamii wana mchango mkubwa katika mafanikio ya sekta mbalimbali kama elimu, afya, na uchumi kwa kubadilisha fikra na kuhamasisha ushirikiano kati ya wananchi na Serikali.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatma Tawfiq, amewapongeza maafisa hao kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuahidi kuwa kamati yake itaendelea kuishauri Serikali kutenga rasilimali zaidi, ikiwemo magari na pikipiki, ili kurahisisha utendaji wao.

Rais wa Chama Cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA), Bw. Victor Kabuje, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwezesha wataalamu hao na kuhimiza ushiriki wa wananchi katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 2025. Aidha, amesema chama hicho kimegawa majiko safi 280 kama sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

No comments:

Post a Comment