Serikali kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) imetoa shilingi bilioni 13.7 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala lenye ghorofa nne na jengo la Maktaba na Maabara ya TEHAMA lenye ghorofa tatu kwa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Kampasi ya Babati mkoani Manyara.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Prof. Eliamani Sedoyeka katika hafla ya kumkabidhi Mkandarasi eneo la ujenzi wa majengo hayo mawili iliyofanyika Mei 06, 2025 Kampasi ya Babati mjini Babati.
Prof. Sedoyeka ameishukuru serikali kwa kuunga mkono jitihada za chuo katika ujenzi wa miundombinu, ambapo amesema pamoja na chuo kujenga majengo mbalimbali kwa kutumia mapato ya ndani; serikali kupitia mradi wa HEET imetoa jumla ya shilingi bilioni 48 kwa IAA, ambapo shilingi bilioni 13.7 zitatumika Babati pekee.
“Uwekezaji uliofanyika katika Kampasi ya Babati unaifanya kuwa miongoni mwa miradi mikubwa mkoani Manyara na utakapoongezewa hizi bilioni 13.7 na utakuwa ni ndio mradi mkubwa kwa mkoa wa Manyara tangu uhuru, tuna mshukuru sana Mhe. Rais Dkt. SAMIA Suluhu Hassan kwa jitihada hizi za kuhakikisha kuwa wana Manyara hawaachwi nyuma katika elimu ya Juu,” alisema Prof. Sedoyeka.
Aidha, Prof. Sedoyeka amesema mradi huo ujenzi unaratajiwa kutekelezwa kwa muda wa miezi 12 chini ya mkandarasi Ami & Vai Investment Ltd na mshauri elekezi Y&P Architect (T) Ltd, ambapo amesisitiza juu ya ubora katika utekelezaji wa mradi huo ili kuendana na matarajio na ndoto za wana Manyara.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga, Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Bw. Halfan Matipula amesema Serikali mkoani Manyara inajivunia uwepo wa IAA; akisisitiza kuwa mradi huo utawanufaisha wakazi wa Manyara wakiwemo wauzaji wa vifaa vya ujenzi, mafundi ujenzi na vibarua, watoa huduma za chakula, malazi,usafirishaji na kuchangia kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Vile vile Bw. Matipula amemtaka Mkandarasi wa atakayetekeleza mradi huo kukamailisha mradi kwa wakati na viwango vinavyotakiwa, ili azma ya serikali ya kupeleka huduma ya elimu kwa wananchi iweze kufikiwa.
Wakati huo huo ametoa wito kwa jamii inayozunguka Kampasi ya Babati pamoja na viongozi kuwa mstari wa mbele katika ulinzi na utunzaji wa vifaa vya ujenzi, miundombinu ya chuo pamoja na wafanyakazi na wanafunzi.
No comments:
Post a Comment