Benki ya CRDB yawakaribisha Wanahisa kwenye Mkutano Mkuu wa 30 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 14, 2025

Benki ya CRDB yawakaribisha Wanahisa kwenye Mkutano Mkuu wa 30


Arusha 14 Mei 2025 - Benki ya CRDB imewataka wanahisa wake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Mkutano Mkuu wa 30 wa Wanahisa, unaotarajiwa kufanyika Jumamosi, tarehe 17 Mei 2025, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya mafanikio tangu kuanzishwa kwa benki hiyo.


Taarifa hiyo imetolewa leo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye hoteli ya Gran Meliá, jijini Arusha, ambapo Benki ya CRDB pia ilizindua Ripoti yake ya Mwaka 2024, inayoonyesha maendeleo makubwa ya kifedha, kiutendaji na kijamii yaliyopatikana katika kipindi hicho.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, amesema kuwa Mkutano Mkuu wa mwaka huu utakuwa wa kipekee kwani utatanguliwa na semina maalum kwa wanahisa na umma, itakayofanyika Ijumaa, tarehe 16 Mei 2025, katika ukumbi wa Simba, AICC. “Semina hii ya kihistoria itakuwa chini ya kaulimbiu yetu ya mwaka huu: ‘Miaka 30 ya Ukuaji wa Pamoja,’ na itafunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango. Ni fursa muhimu ya kutafakari mafanikio yetu ya pamoja, changamoto tulizozishinda, na mwelekeo wetu wa miaka ijayo,” amesema Dkt. Laay.


Ajenda mbalimbali zitajadiliwa katika Mkutano Mkuu wa 30 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ni pamoja na uchaguzi wa wajumbe wa bodi, kuteua wakaguzi wa hesabu, kujadili mapendekezo ya maboresho ya Katiba ya Benki, kujadili na kupokea Taarifa ya Bodi ya Wakurugenzi, na Taarifa ya Hesabu zilizokaguliwa, pamoja na gawio kwa mwaka 2024 ambapo pendekezo la gawio la Sh 65 kwa hisa litawasilishwa sawa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Wanahisa yamekamilika kwa asilimia 100. Nsekela amesema mkutano huo utafanyika kwa njia mseto “Hybrid Meeting” ili kutoa fursa kwa wanahisa wengi zaidi kushiriki moja kwa moja na kwa njia ya kidijitali. “Tumeweka muongozo wa jinsi ya kushiriki mkutano mkuu kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yetu ya www.crdbbank.co.tz, mitandao yetu ya kijamii, lakini pia maelekezo yametumwa kwa ujumbe mfupi kwa Wanahisa,” amesema Nsekela huku akiwahakikishia kuwa Benki hiyo vizuri katika kuhakikisha wanashiriki bila chanagamoto yoyote.

Nsekela amewahamasisha wanahisa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Mkutano Mkuu huo wa kihistoria, akisisitiza kuwa uwepo wao ni muhimu kwa ajili ya kushuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika miaka 30. “Tumejenga taasisi imara inayotoa huduma bora, tumeongeza thamani kwa wanahisa, na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa letu. Hii ni fursa adhimu kwa kila mwanahisa kujivunia sehemu yake katika mafanikio haya na kushiriki kuamua mustakabali wa benki yetu katika miaka ijayo,” amesisistiza.



No comments:

Post a Comment