
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa viongozi wa Mikoa kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za misitu na utafiti kuanzisha bustani za mimea zitakazosaidia kutoa fursa kwa vijana kutafiti na kutengeneza dawa zitakazowasaidia watanzania.
Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati wa Maadhimisho ya Miaka Ishirini ya Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU) yaliyofanyika katika Viwanja vya Chuo hicho mkoani Iringa. Amesema utafiti na utengenezaji dawa kutokana na miti ya asili ni jambo la muhimu hivyo kila mkoa unao wajibu kuhakikisha unalinda miti mbalimbali ya asili na kufanya uhifadhi kwa manufaa ya watanzania.
Pia Makamu wa Rais amesema katika kukabiliana na uhaba wa walimu kwenye Vyuo Vikuu, ni muhimu Taasisi za Vyuo kuendelea kufundisha na kufanya jitihada mahsusi kuwatumia wanafunzi bora wanaopatikana ili waweze kuwa wakufunzi katika vyuo hivyo. Vilevile amewasihi kufanya ushirikiano na Vyuo vya nje ya nchi kwaajili kupunguza uhaba wa walimu katika vyuo vikuu.
Makamu wa Rais amehimiza wanataaluma kuweka mkazo katika tafiti tumizi zinazolenga kukabiliana na changamoto zilizopo katika jamii, kama teknolojia duni na tija ndogo katika sekta za uzalishaji, magonjwa ya binadamu, mimea na mifugo, uharibifu wa mazingira, uongozi-maslahi; siasa chafu, ukatili dhidi ya wanawake na watoto, rushwa na mengineyo. Aidha, ni muhimu pia kwa wanazuoni na wanataaluma kufanya uchambuzi na kujihusisha na mijadala mbalimbali ya kitaifa kwa lengo la kuelimisha jamii na kusaidia utatuzi wa changamoto za muda mfupi au kati na mrefu ikiwemo kutoa mawazo na ushauri kwa Tume ya Rais ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi na ukamilishwaji wa Dira 2050.
Amesema Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma Vyuo Vikuu na vile vya kati. Makamu wa Rais ameongeza kwamba kwa mwaka 2024/25 Serikali ilitenga jumla ya Sh. 254 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wapya wa shahada ya kwanza, ambapo jumla ya wanafunzi 81,079 wamenufaika. Aidha, katika mwaka huo huo, jumla ya Sh. 503 bilioni zimetolewa kwa wanafunzi 157,981 wanaoendelea na masomo katika Shahada ya Kwanza, kwenye Vyuo Vikuu mbalimbali nchini, kikiwemo Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na teknolojia Omary Kipanga amesema Serikali ya Awamu ya Sita, wakati wote imetoa kipaumbele kwa sekta binafsi kushiriki katika uzalishaji na utoaji wa huduma mbalimbali ikiwemo elimu.
Amesema katika kutimiza jukumu hilo Serikali imeendelea kuwekeza katika kujenga mazingira rafiki ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu ya maji, umeme, barabara na mengineyo ili kuhakikisha sekta binafsi zikiwemo Taasisi za elimu zinafanya kazi katika mazingira ambayo ni wezeshi na hivyo kutoa elimu bora na ya ushindani.
Mkuu wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU) ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Romanus Mihali amesema Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linashukuru kwa dhati serikali na wadau wengine ambao wamesaidia katika kukamilika kwa mradi wa jengo la Science Park ambalo linajumuisha Kituo cha Afya.
Amesema lengo ni kuhakikisha Chuo Kikuu Ruaha kinatoa mchango kwa jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya Afya hivyo kuleta mabadiliko chanya kwa jamii kama Taasisi inayohudumia wananchi.
Askofu Mihali amesema bado upo uhitaji wa vifaa tiba ili kituo hicho kianze kutoa huduma kwa wanafunzi, wafanyakazi na wananchi wa mkoa wa Iringa.










No comments:
Post a Comment