DUWASA NA VEI WATOA MISAADA KWA WANAFUNZI 105 WILAYANI KONGWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 16, 2025

DUWASA NA VEI WATOA MISAADA KWA WANAFUNZI 105 WILAYANI KONGWA




Na Okuly Julius – Kibaigwa, Dodoma


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kushirikiana na Shirika la Dutcha Water Operator (VEI) wametoa msaada wa sare za shule na mahitaji ya kujifunzia kwa wanafunzi 105 kutoka shule saba katika Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika kuunga mkono elimu kwa watoto walioko kwenye mazingira magumu.


Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Saimon, amewataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaambia watoto wao kuwa wamefeli mitihani kwa lengo la kukatisha masomo yao, huku sababu kuu ikiwa ni kushindwa kuwahudumia mahitaji ya shule ikiwemo sare.

"Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wazazi wanakata tamaa ya kuwapeleka watoto shule kwa kisingizio cha kufeli, ilhali ukweli ni ukosefu wa sare au vifaa vya shule. Tunapaswa kutafuta njia ya kuwasaidia badala ya kuwakatisha tamaa," amesema DC Mayeka.

Aidha, ameeleza kuwa Wilaya ya Kongwa imetenga kiasi cha Shilingi milioni 20 kila mwaka kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kuhakikisha wanapata elimu bila vikwazo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Bi. Rahel Muhando, amesema taasisi hiyo inatambua wajibu wa kushirikiana na jamii, hasa katika kuunga mkono jitihada za kielimu kwa watoto wa kitanzania.

"Elimu ni msingi wa maendeleo, na tunaamini kila mtoto anastahili nafasi ya kufanikiwa. Huu ni mwanzo wa ushirikiano wetu katika kusaidia jamii ya Kongwa," amesema Bi. Muhando.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa, Mwl. Master Mwashala, pamoja na Mwakilishi wa walimu wakuu kutoka shule zilizopokea msaada, Loishooki Mollel, wameziomba taasisi nyingine kuiga mfano wa DUWASA na VEI kwa kusaidia watoto wanaohitaji msaada ili kufanikisha elimu jumuishi.

Katika tukio hilo, imeelezwa kuwa zaidi ya watoto 450 wilayani Kongwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mahitaji muhimu ya shule. Msaada uliotolewa leo kwa wanafunzi 105 umetajwa kuwa ni hatua ya matumaini kwa kundi hilo katika safari ya kuelekea elimu bila vikwazo.









No comments:

Post a Comment