Na WAF, ARUSHA-Karatu
Mashine sita (6) za kuwasaidia wagonjwa wa dharura katika hospitali ya Halmashauri ya Karatu mkoani Arusha, zimeanza kutumika mara baada ya Madakatari Bingwa wa Rais Samia kutoa mafunzo elekezi kwa watumishi wa hospitali hiyo.
Hali hiyo imebainika Mei 14, 2025 wakati wa zoezi la madaktari bingwa linaloendelea kwenye hospitali ya wilaya hiyo ambapo tayari wananchi wapatao 120 wamejitokeza kwa ajili ya huduma za kibingwa na zile za kawaida.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti watumishi hao wameelezea jinsi madaktari bingwa walivyogeuka walimu na kuwafanikisha kutimiza majukumu yao.
Muuguzi Flomena Joackim akizungumza kwa niaba ya wenzake hospitalini hapo ambaye amefanya kazi katika hospitali hiyo kwa miaka mitatu amedai kuwa alikuwa hajui ni kwa namna gani mashine hizo zinafanya kazi na hivyo waliendelea na majukumu mengine pasipo kuzigusa pamoja na kuwepo hapo.
"Hizi mashine zimekuja zaidi ya miaka miwili (2) iliyopita, lakini tulikuwa hatuna maarifa ya kuzitumia, hivyo tukawa tunatekeleza majukumu mengine na hata tulipopata wagonjwa wa dharura tulilazimika kuwapeleka DDH hospitali ya kanisa," amesema Mary Semurai mmoja wa wauguzi hospitalini hapo.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Usingizi na ganzi Salama Dkt. David Masanja kutoka hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Rukwa amesema toka awasili kituoni hapo ameendelea kutoa mafunzo kwa watumishi namna yakuweza kuendesha mashine hizo za eneo la dharura.
"Hili ni kundi la pili jana nilikuwa nao sita (6) na leo ninao sita (6), ninachoshukuru wanafunzi wangu wameelewa somo vizuri na hata baada ya kambi hii sasa, nadhani hawatatoa tena rufaa kwenda maeneo mengine bali watashughulika nao," amefafanua Dkt. Masanja.
Justina Sumay ambaye ni mmoja ya Wauguzi hakusita kutoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Afya kwa ujumla kwa ubunifu huo wa kusogeza huduma karibu na jamii, lakini pia kuwajengea uwezo watumishi.
No comments:
Post a Comment