Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewataka watendaji wa Tume ya Madini kuongeza ubunifu kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hasa katika kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini kupitia shughuli za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini sambamba na utoaji wa huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
Mhandisi Samamba ametoa kauli hiyo mapema leo Mei 13, 2025 kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa makamishna wapya wa Tume ya Madini jijini Dodoma yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu Sekta ya Madini sambamba na majukumu ya Tume ya Madini. Makamishna wapya walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni pamoja na Mhandisi Theonestina K. Mwasha na Dkt. Theresia C. Numbi.
Amesema kuwa, tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini Aprili, 2018 ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini umeongezeka na kupungua kwa migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kuwataka Makamishna wapya kuendelea kubuni mikakati mipya ya kuhakikisha watanzania wengi wanashiriki kwenye shughuli za madini ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.
“Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana hususan ushiriki mkubwa wa watanzania kwenye Sekta ya Madini na kupungua kwa migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, ninawataka kuongeza ubunifu hasa kwenye usimamizi wa eneo la utoaji wa leseni za madini, ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content) na Wajibu wa Kampuni za Madini kwa Jamii (CSR) ili mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa uendelee kukua,” amesisiza Mhandisi Samamba.
Akielezea mafanikio katika Sekta ya Madini kwa kifupi, Mhandisi Samamba ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa 30, Maafisa Migodi Wakazi 13, Masoko ya Madini 43 na Vituo vya Ununuzi wa Madini 109.
Ameeleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kasi ya ukusanyaji wa maduhuli kuongezeka kutoka shilingi bilioni 164 mwaka 2016/2017 hadi Shilingi 623,237,296,973.40 mwaka 2021/2022, Shilingi 678,042,598,813.92 mwaka 2022/2023 hadi Shilingi 753,175,680,203.96 mwaka 2023/2024, na katika mwaka wa Fedha 2024/2025 hadi mwezi Aprili, 2025 jumla ya Shilingi 875,548,822,865.44 zimekusanywa sawa na asilimia 87.56 ya lengo la kukusanya Shilingi 999,998,000,000.00.
Ameendelea kusema kuwa siri ya mafanikio hayo ni matokeo ya mikakati madhubuti ya Serikali ikiwemo kuimarisha usimamizi wa shughuli za Sekta ya Madini, kudhibiti utoroshwaji wa Madini, kuhamasisha uwekezaji kwenye shughuli za madini na kuanzisha minada ya Madini ya vito.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba amewataka watendaji wa Tume ya Madini kuendelea kusimamia kwa karibu Sekta ya Madini kwa kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi, kusimamia nidhamu na kuongeza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutoa ushirikiano kwa Makamishna wapya na Tume ili Sekta ya Madini iendelee kuwa na taswira chanya na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Wakati huohuo, Mhandisi Samamba amekabidhi vitendea kazi kwa Makamishna wapya ikiwa ni pamoja na miongozo mbalimbali katika usimamizi wa utendaji kazi wa Tume ya Madini.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini. Dkt. Janet Lekashingo akizungumza kwenye mafunzo hayo amewapongeza makamishna wapya kwa uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuahidi ushirikiano kutoka kwa watendaji na watumishi wa Tume ya Madini.
“Kuteuliwa kwenu na Mheshimiwa Rais ni ishara tosha kuwa mna uwezo mkubwa kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini, sisi tunawaahidi ushirikiano mkubwa kwa lengo la kuhakikisha watanzania wananufaika na rasilimali za madini,” amesisitiza Dkt. Lekashingo.
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo ameongeza kuwa Tume ya Madini na watumishi wake itajitahidi na kubuni mikakati bora zaidi ya kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kufanya vizuri kwenye eneo la ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali sambamba na kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini na kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment