
📌 Uwepo wa Umeme Vijijini umeimarisha Usalama
📌 Wananchi wahimizwa kuunganisha umeme kwenye nyumba zao
Wananchi wa Mkoa wa Mtwara wameipongeza na kuishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kukamilisha kufikisha umeme katika Vijiji vyote katika Mkoa huo.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu iliyolenga kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Mikoa ya Kusini.
“Wananchi wa Mtwara wa Vijiji vyote 785 wanafurahia sana uwepo wa umeme katika vijiji vyao. Tunaishukuru sana REA kwa kazi kubwa mnayoifanya. Tungependa kukupongeza wewe kama Mwenyekiti pamoja na Bodi yako ambao mnaisimamia REA na Watendaji wote wa Wakala.
Na zaidi tufikishie salam zetu pia kwa Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Biteko na pongezi za pekee tufikishie kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu haya yote ni maono na matamanio yake. Kwa kweli tunashkuru sana,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Mhe. Kanali Sawala ameongeza kuwa uwepo wa umeme licha ya kuchochea ukuaji wa uchumi, lakini pia umesaidia kuimarisha hali ya usalama hasa ukizingatia Mkoa huo uko mpakani mwa nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa REB, Mhe. Kingu ameendelea kuwahamasisha wananchi kuendelea kufanya maandalizi ya kupokea umeme kwa kusambaza nyaya ndani ya nyumba zao (wiring) katika miradi ya kusambaza umeme katika Vitongoji inayoendelea.
“Dhamira ya Mhe. Rais pamoja na Serikali kwa ujumla ni kuhakikisha kila mwananchi anapata umeme. REA imedhamiria kuhakikisha dhamira hiyo ya Serikali inatimia. Tumemaliza kufikisha umeme katika Vijiji vyote katika Mkoa wa Mtwara na sasa tunaendelea kupeleka katika Vitongoji. Nikuombe Mhe. Mkuu wa Mkoa utusaidie kuwahamasisha wananchi kuupokea umeme pale unapofika kwa kuuingiza ndani ya nyumba zao,” amesema Mhe. Kingu.
Awali akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Mtwara, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu amesema kuwa kuanzia mwaka 2021, Serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 187.7 kwa Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.









No comments:
Post a Comment